Header Ads Widget

KATIBU MKUU CWT TAIFA ATOA MIFUKO 100 YA SARUJI SEKONDARI YA LUGEYE



NA. CHAUSIKU SAID, MATUKIO DAIMA MWANZA 


MWANZA, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Joseph Misalaba, ametoa mifuko 100 ya saruji kwa Shule ya Sekondari Lugeye iliyopo Wilaya ya Magu, Mkoani Mwanza, ili kuanzisha ujenzi wa uzio wa shule hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuondoa changamoto za usalama na uboreshaji wa miundombinu pamoja na kompyuta 10 zitakazowasaidia walimu katika kufundishia somo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Mifuko hiyo ya saruji ameitoa jana Machi 27, 2026, katika Mahafali ya 11 ya Kidato cha Sita, wakati akijibu risala ya wahitimu iliyoeleza changamoto kubwa inayokabili shule hiyo ni ukosefu wa uzio, hali inayohatarisha usalama wa mali za wanafunzi na walimu.

Misalaba ameeleza kuwa kutokana na changamoto hiyo ya ukosefu wa uzio na miundombinu ya bwalo la kulia chakula serikali bado imeendelea kutatua changamoto hizo ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma bila kupata madhara ya aina yeyote.

“Changamoto kubwa niliyoyaona hapa ni ukosefu wa mabweni na uzio. Baada ya kujadiliana na viongozi wenzangu, tuliamua kuwaletea msaada wa mifuko ya saruji na baadhi ya vifaa vya TEHAMA ili kusaidia shughuli za kifundishia na kusomea,” alisema Misalaba.

Mwalimu Florence Kwanama, kutoka Shule ya Sekondari Lugeye, alieleza kuwa shule hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto ya ukosefu wa uzio kwa muda mrefu hali hiyo inatishia usalama wa wanafunzi, hasa wa kike wanaoishi katika mabweni ya shule. 

Kwanama, alisema pia kuwa shule inakosa tanki za maji, vifaa vya TEHAMA kama projecta, televisheni, na spika, pamoja na meza na mabenchi katika ukumbi wa chakula.

“Wanafunzi wetu wa mabweni wanatumia chanzo kimoja cha maji ya uhakika ambacho ni kisimani kinachomilikiwa na kijiji. Pia, tuna upungufu wa paneli za jua mbili ili kusaidia wanafunzi kusoma usiku wakati umeme unapokatika,” alisema Kwanama.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Lugeye, Angela Emmanuel, alikiri uwepo wa changamoto ya uzio na kuomba msaada wa haraka kutoka kwa serikali ili kuimarisha usalama wa wanafunzi.

“Bila kuwa na uzio, wanafunzi wanakuwa hawako salama. Kuna wakati wanafunzi wanapojisomea, watu wasio na nia nzuri wanavunja madirisha na kuingia kwenye mabweni yao kutaka kuiba.”Alisema Angela.

Kwa upande wao, baadhi ya wahitimu wa Kidato cha Sita, Khadija Charles na Victoria Gerald, walisema kuwa ukosefu wa uzio umeleta hofu kubwa kwa wanafunzi, hasa wanapojisomea na kuhofia mali zao kutokuwa salama.

“Wanakuja baadhi ya watu wakati tunajisomea, wanavunja madirisha na kuingia kwa nguvu, wanatuibia vitu vyetu. Hali hii inatufanya tusijisikie salama katika shule yetu,” walisema wahitimu hao.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI