Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imeandaa tamasha maalum litakalojumuisha burudani ya nyama choma pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi.
Akizungumza Machi 4, 2026, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Kibaha Leah Lwanji amesema kuwa tamasha hilo linafanyika katika viwanja vya Stendi ya Zamani Maili Moja, Kibaha, likiwa na lengo la kuwapatia wananchi fursa ya kupata huduma mbalimbali pamoja na kushiriki katika maadhimisho hayo.
Amesema miongoni mwa huduma za kijamii zitakazotolewa ni elimu kuhusu matumizi ya nishati safi, elimu ya fursa mbalimbali za uwezeshaji wanawake kiuchumi, huduma za upimaji wa afya pamoja na uchangiaji wa damu, msaada wa kisheria, na kliniki ya ardhi kwa ajili ya kushughulikia changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya ardhi.
Aidha, maadhimisho hayo pia yameambatana na maonyesho ya bidhaa zinazotengenezwa na wanawake wajasiriamali wa Manispaa ya Kibaha, ambapo wananchi wanapata fursa ya kujionea na kununua bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wajasiriamali hao.
Pia amewaomba Wananchi kutembelea maonyesho hayo kwa lengo la kujionea bidhaa mbalimbali pamoja na kuunga mkono jitihada za wanawake wajasiriamali katika kukuza uchumi wao.
Vilevile, wananchi wote wanakaribishwa kwa wingi kutembelea viwanja vya Stendi ya Zamani Maili Moja Kibaha ili kujipatia bidhaa mbalimbali kutoka kwa wajasiriamali wa eneo hilo, kufurahia nyama choma pamoja na kupata huduma muhimu zinazotolewa katika maadhimisho hayo.








0 Comments