Buzwagi, Kahama
Ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali kuhakikisha inafikia lengo la kuongeza eneo la utafiti kufikia asilimia 50 ifikapo 2030, Waziri wa Madini, *Mh. Anthony Mavunde (Mb)* azindua urushwaji wa Helkopta iliyofungwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya utafiti wa madini nchini.
Amefanya uzinduzi huo leo tarehe 01 Februari, 2026 katika eneo la Buzwagi Wilayani Kahama kuashiria kuanza rasmi utafiti utakaofanywa na Kampuni ya Barrick kwa ajili ya uanzishwaji wa mgodi mpya.
"Kupitia Dira ya Madini 2030: Madini ni Maisha na Utajiri, *Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan* ametuelekeza kuhakikisha tunaongeza eneo la utafiti wa kina wa madini kupitia uwekezaji wa Serikali na Sekta binafsi"
"Tunachokifanya leo hapa ni kiashiria tosha kwamba maono hayo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yanakwenda kufikiwa ipasavyo. Tunaishukuru Kampuni ya Barrick kwa kuamua kuunga mkono juhudi hizi za Serikali kwa vitendo" alieleza Mhe. Mavunde.
Waziri Mavunde pia alibainisha kwamba utafiti huo unaofanywa na Barrick unahusisha helkopta kuruka katika maeneo ya Msalala, Nzega, Igunga, Mbogwe na Nyangh’wale kwa lengo la kupata taarifa zitakazosaidia uanzishwaji wa mgodi mpya.
Kwa maeneo ambayo Barrick itafanya utafiti na kuona hayakidhi vigezo vya uchimbaji mkubwa, Mhe. Mavunde alielekeza kuwa maeneo hayo yatagawiwa kwa wachimbaji wadogo ili kuwaongoza na kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha.
Awali, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Barrick Tanzania, *Dkt. Melkiory Ngido* alibainisha kwamba tangu ianze shughuli zake nchini Tanzania mwaka 2020, Kampuni imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 100 kwenye utafiti wa kina wa madini, na kupitia migodi mitatu inayoiendesha imeweza kuleta nchini thamani ya zaidi ya trilioni 14 kwenye mzunguko wa uchumi wa ndani.
Akitoa Salaam za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, *Mh.Mboni Mhita* aliishukuru Serikali ya *Dkt. Samia Suluhu Hassan* kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini ambayo yamewezesha Kampuni ya Barrick kuendelea kufikiria kuongeza uwekezaji nchini.
Nao wabunge wa Jimbo la Kahama Mjini, *Mh. Benjamin Ngayiwa* na wa Jimbo Msalala, *Mh. Mabula Magangila* wameishukuru Serikali kwa namna inavyowezesha uwekezaji Wilayani Kahama na kueleza matarajio ya wananchi kuwa watakwenda kupata ajira na kuwainua kiuchumi kupitia miradi itakayokwenda kuanzishwa.












0 Comments