Na. Mwandishi Maalum,
WANAWAKE wametakiwa kuzingatia uvaaji wa viatu vyenye kisigino kifupi kuimarisha afya ya miguu na kuepuka kuvaa viatu vyenye kisigino kirefu ama kisigino flati ambavyo ni hatari kwa afya ya magoti.
Hayo yamesemwa na Mtaalamu wa mazoezi tiba kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Jaqline Mariki wakati akizungumza na wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD) katika kambi ya matibabu ya siku mbili ya uchunguzi wa afya iliyofanyika katika ofisi za MSD Kanda ya Mabibo jijini Dar es Salaam.
Jaqline amesema mtu anatakiwa kuvaa viatu vyenye kisigino kifupi ili unyayo uweze kunyanyuka kidogo kusaidia ugawanyishwaji wa uzito kwenye mwili hivyo kutoleta maumivu katika mwili.
“Tunashauri wanawake wasivae viatu virefu au vile ambavyo ni flati bali wavae viatu ambavyo vina kisigino kifupi ili unyayo uweze kunyanyuka kidogo, kwani uvaaji wa viatu vyenye kisigino kirefu unaweza kusababisha ulemavu wa miguu”, amesema Jaqcline.
Aidha, mtaalamu huyo alihimiza wafanyakazi kuwa na utamaduni wa kunywa maji ya kutosha ili kuuweka mwili katika hali bora ya kiafya, akieleza kuwa ukosefu wa maji mwilini unaweza kusababisha maumivu ya kichwa, uchovu na kupungua kwa ufanisi wa kazi.
“Kama tunavyofahamu wafanyakazi wengi maofisini hawapendelei kunywa maji mengi kwasababu muda mwingi wanautumia wakiwa wamekaa, jambo ambalo linaweza kusababisha maumivu ya kichwa na kupunguza ufanisi wa kufanya kazi”, aliongeza Jaqckline.
Kwa upande wao wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD) waliopatiwa mafunzo hayo wameshukuru kwa kupatiwa uelewa mpana kuhusu afya ya moyo, viungo vya mwili pamoja na matumizi sahihi ya dawa za kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
“Nilikuwa sifahamu kabisa kama ugonjwa wa homa ya ini unaweza kusababisha saratani, kupitia mafunzo hayo nitahakikisha nakuwa makini kwa kuchukua hatua ya kupima na kupata chanjo”, amesema Haika Regnald
“Binafsi mafunzo haya na upimaji huu ni fursa nzuri kwangu kuweza kujua hali yangu ya moyo, kisukari na uzito kwani katika mafunzo haya tumesisizwa kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ya mara kwa mara” amesema Ally Mlete.









0 Comments