Na. Matukio Daima Media App, Zanzibar.
MSANII wa singeli Man Fongo ameweka wazi kuwa anaingia 'chimbo' kuandaa nyimbo zenye jumbe maalum za kutetea haki za Wanawake na Watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Man Fongo amesema hayo katika mjadala ulioandaliwa na UNICEF kwa kushirikiana na Sauti za Busara, uliojikita katika namna wasanii wanavyoweza kutumia sauti na ushawishi wao kukemea ukatili na kutetea haki za wanawake na watoto.
Mjadala huo uliwakutanisha wasanii, wadau wa sanaa na wataalamu wa ulinzi wa watoto kutoka UNICEF, kwa lengo la kuhimiza utengenezaji wa kazi zitakazoishi vizazi na vizazi.
Aidha, Man Fongo ameshukuru Sauti za Busara kwa kuweza mkutanisha na wadau katika tasnia ya muziki hali ambayo inafanya muziki wake kwenda mbali.
mjadala huo umempa msukumo mpya wa mwelekeo wa kazi zake na kuwa na matamanio ya kuandaa nyimbo zitakazotetea haki za wanawake na watoto na kupinga vitendo vya ukatili.
“Nitatumia muziki mzuri kuwafikishia watu ujumbe,” amesema na kuongeza : “Wasanii tuna nafasi ya kuelimisha jamii kuhusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto kupitia nyimbo zinazopendwa na wengi.”
Ameongeza kuwa, maudhui atakayoyazalisha yatazungumzia masuala yanayogusa rika lake na vizazi vilivyotangulia, huku yakilenga pia kufikia hadhira pana na kuwa na mvuto katika majukwaa ya kidijitali.
Akihitimisha mjadala huo, Mkuu wa Ulinzi wa Watoto wa UNICEF, Miranda Armstrong amesema wasanii wana jukumu kubwa la kusukuma mbele ujumbe unaolinda haki za watoto.
“UNICEF imefanya kazi na mabalozi wengi wa haki za watoto, na wasanii wamekuwa sehemu ya safari hiyo,” amesema.
“Tunasubiri kuona wasanii wengi zaidi wakijitokeza kuwa mabalozi wa vijana na watetezi wa haki za watoto.”
Kwa ujumla, mjadala huo uliweka wazi jambo moja muhimu: zaidi ya burudani, muziki ni chombo chenye nguvu ya kuunda maadili ya jamii—na wasanii wana nafasi ya kipekee kutumia sauti zao si tu kuiburudisha jamii, bali pia kulinda mustakabali wake

-54.jpg)






















0 Comments