Dodoma
Imeelezwa kwamba, ushiriki wa Sekta ya Madini Tanzania katika Kongamano la Kimataifa la Mining Indaba lililofanyika kuanzia tarehe 8 – 12 Februari, 2026, jijini Cape town nchini Afrika Kusini, limeibua fursa mpya za uwekezaji kufuatia ujumbe wa Tanzania kukutana na wadau muhimu wa kimataifa ambao wameonesha nia ya kuanzisha michakato ya uwekezaji na ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali.
Hayo yamebainishwa katika taarifa iliyotolewa kwa umma na Wizara ya Madini Februari 18, 2026 iliyoainisha maeneo muhimu yaliyojadiliwa ya uongezaji thamani madini ambapo wameeleza utayari wa kushirikiana katika kutimiza ndoto ya Tanzania na Afrika kusukuma agenda ya kuongeza thamani madini ndani ya nchi kwa kuanzisha viwanda badala ya kusafirisha madini ghafi, uendelezaji madini muhimu na mkakati, na ushirikiano kwenye utafiti wa kina wa madini.
‘’Masuala mengine yaliyopewa umuhimu ni kuwajengea uwezo wataalam katika masuala ya madini, teknolojia za kisasa na utunzaji wa taarifa na takwimu za jiosayansi pamoja na Tanzania kunufaika na program ya PanaAfGeo+ kupitia Umoja wa Ulaya inayolenga kuimarisha uwezo kwenye masuala ya utafiti wa jiolojia na kuhawilisha ujuzi kwa watumishi wa umma katika Sekta ya Madini,’’ imeeleza taarifa hiyo.
Pia, taarifa hiyo imeeleza kuwa, hotuba ya Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde aliyoitoa siku ya pili ya kongamano hilo, imetoa nafasi kubwa kwa Tanzania kuzibainisha fursa zake za uwekezaji, ikiwemo kutoa mwelekeo wa Sekta ya Madini Tanzania na kutoa uelewa na ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kisekta.
‘’kupitia kongamano hilo, Sura ya Tanzania kwenye Sekta ya Madini imeendelea kuwa ya kuvutia na kuchukua nafasi nzuri kutokana na namna Serikali inavyosimamia Sekta ya Madini; mafanikio yaliyopatikana kwenye Sekta ya Madini; namna Serikali inavyojenga uwezo wa ndani ; urasimishaji wa sekta ndogo ya uchimbaji mdogo wa madini, na mikakati ya ushirikishwaji wa watanzania katika uchumi wa madini.’’ Imesema taarifa hiyo .
Vilevile, taarifa hiyo imeeleza kwamba, warsha zilizoandaliwa na kampuni ya Breakthrough Attorneys inayotoa huduma mbalimbali za kisheria kimataifa, kwa kushirkiana na benki ya NMB, na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), warsha ya Kampuni ya Faru Graphite, Chemba ya Migodi Tanzania (TMC) na ushiriki wa wadau wengine kwenye midahalo wakati wa kongamano zilichangia kuitangaza nafasi ya Tanzania kimataifa kama kimbilio la uwekezaji Afrika kwenye Sekta ya Madini.
Ujumbe wa Tanzania katika kongamano hilo ukiongozwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ulijumuisha wataalamu kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zake, TISEZA, pamoja na wadau wa Sekta binafsi wakiwemo Chemba ya Migodi Tanzania (TCM), Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Tanzania (FEMATA), Umoja wa Vijana Wachimbaji Tanzania (TYM), Chama cha Wanawake na Vijana katika Uchimbaji na Sekta ya Madini (TWiMMI), Kampuni za uchimbaji madini, taasisi za fedha, watoa huduma migodini na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa madini.






.jpg)




.jpg)




0 Comments