Header Ads Widget

AMANI NI MUHIMILI WA UHAI NA MAENDELEO YA BINADAMU- MWAIKASU



 Wito umetolewa kwa Jamii kuafikiana na kupendelea njia ya mazungumzo katika utatuzi wa migogoro mbalimbali, Vijana wakitakiwa pia kujiepusha na vikundi visivyokuwa na tija kwa ustawi wao pamoja na kukataa kujihusisha na maneno na matendo yenye kuashiria uvunjifu wa amani kwani amani ndio muhimili wa uhai na maendeleo ya binadamu.

Aidha Watanzania pia kwa imani zao tofauti wamesisitizwa umuhimu wa kumshirikisha na kumuomba Mwenyenzi Mungu aendelee kuibariki na kuidumisha amani ya Tanzania, mifano ikitolewa kwa namna ambavyo baadhi ya Mataifa duniani yalivyopitia madhila makubwa ya kijamii na kiuchumi kutokana na kutoweka kwa amani katika mataifa hayo licha ya jitihada nyingi zilizoshindwa za kuirejesha amani katika mataifa hayo.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Jumanne Februari 17, 2026 Bi. Aneth Dickson Mwaikasu, Mkazi wa Kigogo Fresh, Jijini Dar Es Salaam amekumbusha pia umuhimu wa amani katika maendeleo na ustawi wa Jamii, akisema amani ni tunu muhimu na ya mfano ambayo Tanzania imebarikiwa kuwa nayo na hivyo ni muhimu kuilinda na kuiendeleza.

"Sisi kama binadamu tunamuhitaji Mungu sana ili amani yetu aliyoitunuku Tanzania yetu iendelee kuwepo na cha pili lazima tuafikiane kama binadamu kwamba tufanye nini ili amani iendelee kuwepo kwasababu amani hainunuliwi na ikipotea kuirudisha haijawahi kuwa rahisi ama kuwezekana hata kidogo." Amesema Bi. Mwaikasu.

Serikali ya Tanzania inaichukulia amani si dhana pekee bali kama hitaji la msingi ambalo bila hilo hakuna anayeweza kupata maendeleo ambapo msingi huo pia unaungwa mkono na Umoja wa Mataifa ambapo kulingana na malengo ya maendeleo endelevu, amani ni kigezo cha kwanza cha kufikia malengo mengine yote duniani, ikisema jamii zenye amani ndizo zinazoweza kupunguza rushwa, kutoa haki sawa kwa wote na kukuza uwajibikaji kwa jamii.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI