Waziri Kijaji atoa dira ya “Kazi na Utu”, ataka mageuzi ya uhifadhi, nyuki na utalii wa misitu
Dodoma, Februari 13, 2026 – Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS umeandika ukurasa mpya katika historia ya usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki baada ya kuzindua rasmi Bodi yake ya Tano ya Ushauri katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Best Western, Dodoma.
Uzinduzi huo ulifanywa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, aliyetoa maelekezo mazito na ya kimkakati kwa bodi hiyo, akisisitiza ufanisi, uwajibikaji na utekelezaji wa kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Sita ya “Kazi na Utu”.
Bodi mpya, matumaini mapya
Bodi hiyo inaongozwa na Luteni Mstaafu Chiku Abdallah Sumbu Gallawa, ambaye amepewa jukumu la kuisimamia TFS katika kuishauri Wizara kuhusu utendaji wake, kwa lengo la kuongeza tija, uwazi na mchango wa sekta ya misitu katika uchumi wa taifa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Dkt. Kijaji aliwataka wajumbe wa bodi kutumia uzoefu wao mkubwa kuhakikisha TFS inageuza changamoto zilizopo kuwa fursa za maendeleo.
“Nini tufanye ili tugeuze namba za upotevu wa misitu? Hilo ni jukumu lenu. Hakikisheni tunalinda rasilimali hizi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisisitiza Waziri.
Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa, Tanzania ina takribani hekta milioni 48.1 za misitu, sawa na asilimia 55 ya eneo la Tanzania Bara, ambapo TFS inasimamia takribani hekta milioni 12.5.
Kipaumbele: Uhifadhi shirikishi na teknolojia
Waziri alielekeza bodi kuhakikisha matumizi ya teknolojia yanaongezwa, ikiwemo satelaiti na ndege zisizo na rubani (drones), ili kuimarisha ufuatiliaji wa misitu na kudhibiti vitendo vya uhalifu mapema.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa usimamizi unaozingatia utu kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi, akibainisha kuwa kulinda misitu hakupaswi kwenda sambamba na kuharibu mahusiano ya kijamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi, Luteni Mstaafu Gallawa, aliahidi kuwa bodi itafanya kazi kwa weledi, uwazi na kwa kushirikiana na wadau wote.
“Sisi ni sehemu ya jamii. Tutashirikiana na wananchi na taasisi nyingine kuhakikisha tunafikia matokeo chanya,” alisema.
Nyuki: Fursa ya uchumi na suluhisho la migogoro
Katika maelekezo yake, Waziri aliipa uzito mkubwa sekta ya nyuki, akieleza kuwa ni eneo lenye uwezo mkubwa wa kuongeza kipato cha wananchi na kupunguza utegemezi usio endelevu wa misitu.
TFS imeelekezwa kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki, kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata asali, na kuunganisha uzalishaji na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mkakati huo unatarajiwa kuongeza ajira, kipato cha jamii zinazozunguka misitu, na kuchochea uhifadhi endelevu.
Utalii wa misitu kuelekea watalii milioni 8
Waziri pia aliielekeza bodi kuimarisha utalii wa ikolojia katika maeneo ya misitu, akihusisha juhudi hizo na azma ya taifa ya kufikia watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030 chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kupitia filamu za kimataifa za Tanzania: The Royal Tour na Amazing Tanzania, Tanzania imeendelea kujitangaza kama kitovu cha utalii wa asili. TFS imejipanga kuibua vivutio vipya vya misitu kila mwaka na kuvifungamanisha na malengo ya idadi ya watalii.
Dira ya TFS: Tija, Taswira na Utu
Katika hotuba yake, Dkt. Kijaji alisisitiza kuwa pamoja na mchango wa mapato kwa Serikali, TFS inapaswa kujenga taswira chanya kwa jamii na kujiwekea viashiria vya kupima kiwango cha kukubalika kwake.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe, Mwenyekiti wa Bodi, Luteni Mstaafu Gallawa, alimhakikishia Waziri kuwa bodi itatekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa kuzingatia ushirikishwaji wa wananchi.
“Hatutaona jamii kama wapinzani. Sisi pia ni sehemu ya jamii. Tutashirikiana na taasisi na wizara nyingine ili kutoa matokeo chanya,” amesema.
Awali, akimwakilisha Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Wizara ya Maliasili na Utalii, Bernard Patrice Marcelline, alisema TFS ilianzishwa kwa Sheria ya Wakala Sura 245 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali mwaka 2010, ikiwa ni bodi ya tano tangu kuanzishwa kwake.
Disemba 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alimteua Luteni Mstaafu Chiku Abdallah Sumbu Gallawa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), huku Waziri Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akiteua wajumbe ambao ni:
Bw. Daniel Charles Pancras, Bw. Godwin Kowero Sifael, Prof. Peter Reuben Gillah, Bw. Stephen Wangias Mariki, Bi. Zainab Peter Kuhanwa na Prof. Dos Santos Aristarick Silayo (Katibu wa Bodi). Uteuzi ulianza Desemba 5, 2025 na Bodi itahudumu hadi Desemba 4, 2028.













0 Comments