Morogoro.
Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), kwa kushirikiana na Missouri Botanical Garden ya Marekani, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), imepanga kutekeleza mradi wa miaka mitatu wa kuhifadhi spishi za miti adimu na zilizo hatarini kutoweka nchini. Mradi huu unafadhiliwa na Taasisi ya Fondation Franklinian na unalenga kuimarisha uhifadhi wa spishi za miti 57 iliyo katika hatari kubwa ya kutoweka nchini.
Mazungumzo kuhusu mashirikiano ya mradi huu yamefanyika Februari 06, 2026 TAFORI Makao Makuu, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt. Revocatus Mushumbusi, alifungua rasmi kikao hicho na kupokea mawasilisho ya mradi kutoka kwa watafiti wa Missouri Botanical Garden wakiongozwa na Dkt. Roy Gereau na Dkt. Tariq Stevart. Mradi huo unaitwa _“Kuimarisha Uhifadhi wa Miti Iliyo Hatarini Kutoweka Nchini Tanzania”_ (Enhanced Conservation of Highly Threatened Tanzanian Trees).
Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa katika maeneo ya kati na kusini mwa Milima ya Tao la Mashariki ukilenga uhifadhi wa spishi adimu za miti ya asili kama vile _Gigasiphon macrosiphon_, na _Garcinia semseii_, ambazo zina mchango mkubwa katika uhifadhi wa bayoanuai na pia zina thamani katika tafiti za kisayansi na kiuchumi kwa jamii zinazozunguka misitu, hususani katika matumizi ya mbao na utengenezaji wa samani.
Hatua kuu za utekelezaji wa mradi huu ni pamoja na ufuatiliaji wa spishi porini, majaribio ya uoteshaji wa miche, pamoja na uanzishaji wa vitalu vya miche vinavyoendeshwa na jamii kwa lengo la kurejesha idadi ya miti hiyo katika mazingira yake ya asili.
Tanzania inakadiriwa kuwa na zaidi ya spishi 1,800 za miti ya asili, ambapo takribani spishi 378 zinakabiliwa na hatari ya kutoweka. Hali hii inatokana na changamoto mbalimbali ikiwemo uharibifu wa misitu, mabadiliko ya tabianchi na shinikizo la shughuli za kibinadamu, hali inayofanya juhudi za uhifadhi wa miti adimu kuwa za umuhimu mkubwa kitaifa.
Ushiriki wa TAFORI katika mradi huu unatokana na jukumu lake kuu la kufanya, kuratibu na kusambaza matokeo ya utafiti wa misitu na ufugaji nyuki hapa nchini Tanzania.












0 Comments