Mwelekeo na kasi Mpya katika Uhifadhi, Utalii na Kuleta Ufanisi wa Kiutendaji.
Na. Jacob Kasiri - Dodoma.
Katika hatua muhimu ya kuimarisha utendaji anuwai wa TANAPA na kuweka mwelekeo wa maendeleo ya miaka mitano ijayo, timu ya wataalamu iliyokuwa inafanya marejeo na hatimaye kuandaa Mpango Mkakati Mpya kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imewasilisha rasmi rasimu ya Mpango Mkakati 2026/2027 –2030/2031 kwa Bodi ya Wadhamini - TANAPA iliyokuwa inaongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Majeshi (Mst). Jen. George Waitara leo Februari 07, 2026 katika Ukumbi wa Ofisi Kiunganishi ya TANAPA uliopo jijini Dodoma.
Uwasilishwaji huo umefanyika katika kikao maalumu kilicholenga kupitia kwa kina Malengo Makuu Saba yaliyowekwa katika Mpango Mkakati huo mpya wa Taasisi, vipaumbele vya kimkakati pamoja na mikakati ya kuboresha uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori na mimea, kuwa na utalii endelevu na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wadau.
Akizungumza wakati wa upokeaji rasmi wa Mpango Mkakati huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini - TANAPA, Mkuu wa Majeshi (Mst.) Jen. George Waitara aliipongeza timu hiyo kwa hatua nzuri waliyofikia na kuwataka maoni na ushauri utakaotolewa na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini kuuzingatia sanjari na kuyajumuisha katika mpango huo ili kuleta tija katika utekelezaji wa majukumu yake yatakayochangia katika kuendeleza sekta ya Uhifadhi na utalii kwa ajili ya faida ya sasa na vizazi vinavyokuja.
Aidha, Jen. Waitara aliongeza kuwa Mpango Mkakati huu umegusa kila mahali na ni wa miaka mitano tu ukitarajiwa kuanza kutumika rasmi kuanzia Julai mosi 2026 hadi June 30, 2031, niwasihi ninyi ni wataalamu wa uhifadhi sasa fikirieni kuja na Mpango Mkakati wa muda mrefu mkilenga miaka 100 ijayo. Tufikilie rasilimali hizi zitakuwaje baada ya miaka 100, na mje na mkakati wa kuishauri serikali namna bora ya kuendelea kuwa na Hifadhi za Taifa zilizosheni wanyamapori na mimea kama ilivyo sasa. Isije ikatokea baada ya miaka 100 ijayo tukawa na hifadhi zisizo na wanyamapori.
Akielezea mchakato wa uandaaji wa Mpango Mkakati huo mpya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Sekela Mwangota - Mkuu wa Kitengo cha Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini - TANAPA ambaye ni Msimamizi wa timu ya wataalamu waliofanikisha Mpango Mkakati huo alisema,
“Mpango Mkakati huu Mpya umeandaliwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) 2025 hasa katika lengo lake la kufikisha watalii milioni nane ifikapo june 2030, Sera mbalimbali za Taifa na Hotuba ya Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13 Novemba 14, 2025 jijini Dodoma.”
Akiwasilisha Mpango Mkakati huo, Dkt. Wilhelm Kiwango Mhadhiri kutoka Chuo kikuu Dodoma ambaye ni mtaalamu mwezeshaji alieleza mafanikio yaliyofikiwa katika Mpango Mkakati 2020/2021 - 2025/2026 unaelekea kutamatika yakiwa ni pamoja na matumizi ya TEHAMA kupunguza upotevu wa maduhuli na utoaji wa huduma kwa watalii uliorahisishwa kutoka dakika 5 za awali na kufikia chini ya dakika 3 kwa sasa.
Aidha, Dkt. Kiwango aliongeza, “TANAPA imefanikiwa kwa 100% kukabiliana na matukio yote yaliyoripotiwa ya kuzuia migogoro kati ya binadamu na wanyamapori sambamba na matumizi ya sayansi na teknolojia yaliyochagiza ongezeko la wanyamapori wakubwa waliokuwa hatarini kutoweka ambao ni faru weusi, sokwemtu pamoja na mbwamwitu katika Hifadhi za Taifa Mkomazi, Serengeti, Rubondo Mahale na Gombe.”
“Katika Mpango Mkakati Mpya utaendeleza mazuri yote yaliyokuwa yakiendelea chini ya mkakati unaomaliza muda wake na kwenda mbali zaidi kuimarishi ulinzi wa maliasili, ikolojia na kutoa huduma bora kwa watalii ili waweze kurudi tena na tena katika hifadhi zetu tofauti na ilivyo sasa aliongeza Dkt. Kiwango.
Baada ya wasilisho hilo michango na hoja mbalimbali muhimu ziliwasilishwa na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini TANAPA wakiwemo CPA Hadija Ramadhani, Dkt. Robert Fyumagwa, Bw. Athumani Kwariko pamoja na Dkt. Fortunata Msoffe ambapo timu ya wataalamu hao imeafiki kuyafanyia kazi na hatimaye kuyajumuisha katika Mpango Mkakati huo wa 2026/27 - 2030/31.












0 Comments