Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu itaendelea kuimarisha na kuboresha ushirikiano na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika kuimarisha tafsiri sahihi ya sheria.Mwanasheria Mkuu wa Serikali amezungumza hayo wakati alipokuwa mgeni rasmi katika halfa ya Iftari iliyoandaliwa na NEMC tarehe 26 Februari, 2026 Jijini Dar es Salaam.
*“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu itaendelea kushirikiana nanyi katika kuimarisha tafsiri sahihi ya sheria, pamoja na kuhakikisha kuwa hatua za kisheria zinachukuliwa pale inapobidi kulinda maslahi ya Taifa.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Aidha, Mhe. Johari amesisitiza kuwa suala la Mazingira si suala la hiari bali ni wajibu wa kisheria na wa kimaadili, pia ameeleza kuwa utekelezaji madhubuti wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na kanuni zake ni muhimu katika kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanaenda sambamba na ustawi wa jamii na uhifadhi wa rasilimali kwa vizazi vijavyo.
*“Katika hili, NEMC mna jukumu kubwa la kusimamia utekelezaji wa sheria hizo kwa weledi, haki na bila upendeleo.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali .
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewapongeza NEMC kwa kuandaa hafla hiyo ya Iftar ambayo imewaleta pamoja viongozi, watumishi na wadau mbalimbali wa Sekta ya Mazingira.
*“Matukio kama haya huimarisha uhusiano wa kitaasisi na kujenga ari mpya ya kulitumikia Taifa kwa bidii na uadilifu.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NEMC Bw. Alex Mgongolwa amesema kuwa Bodi ya Wakurugenzi itaendelea kuisimamia Menejimenti ya NEMC ili kuhakikisha kuwa NEMC inatekeleza wajibu wake kwa ufanisi, kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya nchi. Vilevile, bodi hiyo itaendelea kuimarisha mifumo ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji ili taasisi hiyo iwe mfano wa kuigwa katika sekta ya umma.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware amemshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo ya Iftrai ambapo amesema kukubali kwake kua mgeni rasmi kunaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha misingi ya utawala wa sheria katika usimamizi wa mazingira.
*“Tunathamini sana mwongozo na msaada tunaoupata kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kuimarisha misingi ya uwajibikaji na haki katika sekta ya mazingira.”* Amesema Dkt. Sware





0 Comments