Mkaguzi wa Polisi Raymond Mutalemwa, anayehudumu kama Polisi Kata ya Ifunda katika Tarafa ya Kiponzero, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, amewasisitiza wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Ifunda (Ifunda Girls) umuhimu wa kutoa taarifa mapema pindi wanapobaini au kushuku dalili za vitendo vya ukatili, ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati.
Akizungumza na wanafunzi hao, Mkaguzi Mutalemwa alieleza kuwa mara nyingi vitendo vya ukatili huanza na viashiria vidogo vinavyopuuzwa, hivyo ni muhimu kwa wahanga au mashuhuda kuwa jasiri na kutoa taarifa bila hofu.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kulinda usalama wa watoto na wanafunzi, na kwamba taarifa zote zinazotolewa hushughulikiwa kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia usiri.
Elimu hiyo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto na wanafunzi shuleni, ambapo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya shule, jamii na Jeshi la Polisi katika kupambana na vitendo vya ukatili.








0 Comments