Na Calvin Katera - Moshi
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limekutana na kufanya kikao kazi na wamiliki wa makampuni ya Helikopta za uokoaji (helikopta) kwa lengo la kuimarisha mahusiano na ushirikiano wa pamoja katika uendeshaji wa shughuli za uokoaji ndani ya Hifadhi za Taifa, hususan Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro.
Kikao hicho kimefanyika leo Februari 03, 2026 mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, kikijikita katika kujadili maboresho ya huduma za uokoaji, usalama wa wageni pamoja na ufanisi wa utoaji wa huduma za dharura za kiafya kwa wageni wanaotembelea hifadhi hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Kaskazini Steria Ndaga amesema kuwa wamiliki wa makampuni ya Helikopta za uokoaji ni wadau muhimu katika kulinda usalama wa wageni na kuchangia maendeleo ya hifadhi. Alieleza kuwa huduma za uokoaji za haraka na zenye ufanisi ni nguzo muhimu katika kuokoa maisha ya wageni pindi dharura za kiafya zinapojitokeza.
“TANAPA imelenga kuendelea na kukuza ushirikiano ambao tumekuwa tukiujenga kwa muda mrefu na wadau hawa, ili kuhakikisha huduma za uokoaji zinawafikia walengwa kwa wakati. Tumeendelea kuweka mazingira rafiki ya utekelezaji wa shughuli zenu, ili kuhakikisha wageni wanaougua ndani ya hifadhi, hususan Mlima Kilimanjaro, wanapatiwa huduma ya haraka na ya uhakika kwa lengo la kuokoa maisha yao,” alisema Kamishna Ndaga.
Kwa upande wake, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Angela Nyaki, alisema kuwa wadau wa uokoaji wana mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa wageni na kukuza sekta ya utalii. Aliongeza kuwa utoaji wa huduma bora na za haraka za uokoaji utasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na changamoto za kiafya na mabadiliko ya hali ya hewa mlimani.
Naye Afisa Mwandamizi wa Uhifadhi, Washington Idrissa, aliwataka wadau wote wa uokoaji kuzingatia kikamilifu taratibu na miongozo ya kiusalama inayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Anga Tanzania (TCAA). Amesisitiza umuhimu wa kuzingatia masuala ya usalama wa vyombo vya uokoaji, mafunzo kwa marubani, pamoja na upatikanaji wa vibali halali vya kufanya shughuli za uokoaji ndani ya hifadhi bila kukiuka sheria na taratibu zilizopo.
Aidha, Ndugu Ben Simpson Mdau kutoka kampuni ya Tropic Helicopters amewahimiza watoa huduma wote wa uokoaji kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na TCAA na TANAPA. Alisema kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, uwazi na heshima kwa wadau wengine kutasaidia kuondoa migongano ya kimaslahi na kuongeza ufanisi wa huduma za uokoaji.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wadau wa huduma za uokoaji kwa kutumia ndege (helikopta) kutoka makampuni ya Pro Flights Limited, Tropic Helicopters, Level Up Aviation na Kilimedair na TANAPA kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuboresha usalama wa wageni ndani ya Hifadhi za Taifa, hususan Mlima Kilimanjaro.













0 Comments