Na. Jacob Kasiri - Dodoma.
Timu ya wataalamu wabobezi kutoka katika Idara na Vitengo mbalimbali vya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wapo jijini Dodoma kuanzia Februari 02, 2026 kwa ajili ya kufanya marejeo na hatimaye kuandaa Mpango Mkakati Mpya (Strategic Plan) wa Miaka Mitano ijayo 2026/2027 - 2030/2031 baada ya Mpango Mkakati wa awali 2020/2021 - 2025/2026 kuelekea ukingoni ifikapo June 31, 2026.
Lengo la Mpango Mkakati huo ni kubainisha mwelekeo wa kimkakati na vipaumbele vya taasisi hiyo inayosimamia Hifadhi za Taifa 21, vituo vitano vya Malikale pamoja na Ofisi Viunganishi tatu za Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar ili kutekeleza majukumu yake kwa uwazi, uwajibikaji na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi - Sekela Mwangota Mkuu wa Kitengo cha Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini - (TANAPA) ambaye ni Msimamizi Mkuu wa maandalizi ya (SP) hiyo mpya alisema,
“Mpango Mkakati huo unalenga kuongeza mazao mapya ya utalii, uimarishwaji wa ikolojia ikihusisha tiba za wanyamapori, upatikanaji wa maji ya kutosha katika Hifadhi za Taifa zinazokabiliwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya Tabianchi kama vile Mikumi, Mkomazi, Katavi na Saadani sanjari na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili shirika liendee na shughuli zake za uhifadhi hata kama nchi itakabiliwa na majanga yatakayosababisha watalii kutokuja nchini kama ilivyotokea wakati wa Uviko 2019.”
Aidha, Kamishna Sekela aliongeza kuwa Rasimu ya Mkakati huo imejikita kuweka mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ikianza na hali ya awali kabla ya mpango (baseline) pamoja na malengo ya kufikiwa na Idara au Kitengo kwa kila mwaka (targets). Tathmini hizo zitafanyika kwa kuangalia (ripoti ya utendaji kazi wa kila dawati, tafiti, kiwango cha kuridhika kwa wateja wetu na takwimu) lengo likiwa ni kupima kama taasisi inasonga mbele kuelekea kufikia malengo yake au la!.
Dkt. Wilhelm Kiwango Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma ambaye ni mwezeshaji katika zoezi la uandaaji wa Mpango Mkakati Mpya (SP) alitanabaisha kuwa ili kupata Mpango Mkakati suluhishi utakaokidhi na kufikia malengo tarajiwa ya TANAPA, mambo muhimu yaliyoangaziwa ni pamoja na uainisha wa takwimu na uzoefu wa kitaaluma, kubaini maeneo ya kimkakati yatakayopewa kipaumbele katika miaka mitano ijayo, pamoja na matumizi bora ya rasilimali vifaa na watu ambayo itaenda sambamba na kasi ya utoaji huduma kwa wateja.
Upatikanaji wa Mpango Mkakati (SP) huo utakuwa ni mwelekeo thabiti wa TANAPA kufikia Malengo yake kuendana na mazingira ya sasa, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, miongozo mbalimbali ya serikali inayochagizwa na sera, kanuni, mwelekeo mpya na kasi ya Wizara ya Maliasili na Utalii.



.jpg)





0 Comments