Na. Joyce Ndunguru, Morogoro.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mej.Jen (Mst) Hamis Semfuko amefungua rasmi Kikao cha 33 cha Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA kilichofanyika Februari 17,2026, Mkoani Morogoro.
Akizungumza katika Kikao hicho ambacho ni Kikao cha kwanza cha Bodi ya Nne iliyozinduliwa rasmi mnamo Januari 10, 2026, na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt Ashatu Kijaji, Mej.Jen (Mst) Semfuko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kwa mara ya pili kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA.
Aidha, amewapongeza Wajumbe wa Bodi ya Nne kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Dkt Ashatu Kijaji.
Sambamba na pongezi hizo, Mej.Jen (Mst) Semfuko amesema Bodi hii ya Nne ina jukumu la kuhakikisha TAWA inazidi kukua na kupaa kwa viwango vya ubora na ufanisi katika nyanja zote ikiwemo kuimarisha ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori katika maeneo ya hifadhi pamoja na kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato.
Pia, kuimarisha miundombinu ya utalii, matumizi ya mbinu za kisasa katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu na kuendelea kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya watumishi.
Pamoja na ufunguzi huo, Bodi ya Wakurugenzi imepata fursa ya kupitia taarifa ya mapitio ya Bajeti ya Taasisi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na kupitia taarifa zingine za kamati mbalimbali.




















0 Comments