Header Ads Widget

MAKAMU WA RAIS DKT NCHIMBI AONGOZA MAADHIMISHO YA MIAKA 49YA CHAMA CHA MAPINDUZI


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM na Mlezi wa CCM Mkoa wa Dodoma, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amewaasa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba wanatimiza wajibu wa msingi na wa kudumu wa kuhakikisha CCM inakuwa chama cha Watanzania na kimbilio lao.

Makamu wa Rais, amesema hayo wakati akiongoza Maadhimisho ya Miaka 49 ya Chama Cha Mapinduzi, yaliyofanyika Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, leo tarehe 05 Februari 2026. Amesema wakati CCM ikitimiza miaka 49 bado Watanzania wana imani na Chama hicho, imani iliyodhihirishwa kwa kuchaguliwa kuongoza Nchi.

Makamu wa Rais amesema, kila mwanachama na kiongozi wa CCM anapaswa kutafakari kila anachofanya au kutenda kitachangia vipi kuleta maendeleo, umoja na utengamano wa CCM na Taifa kwa ujumla.

Amesema ni lazima kwa Viongozi wakiwemo Wabunge, Madiwani, Viongozi wa Vitongoji na Mitaa kuibeba na kuisimamia Ilani ya CCM kwani imetafsiri kwa vitendo nia ya Chama hicho kuleta maendeleo.


Aidha, amesema Chama hicho kinapaswa kuendelea kuwa mfano wa siasa safi, kwa kujiepusha na siasa za fitina na kuchafuana. Ameongeza kwamba ni muhimu wanachama wa CCM wote kwa matendo na maneno yao kuhakikisha wanajenga chama hicho.

Makamu wa Rais amesema ni vema kutambua msingi wa Chama Cha Mapinduzi ni watu, umoja, maendeleo na utumishi. Amewataka wanachama kuitekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 49 ya Chama hicho ambayo ni “Tumechagua Umoja na Amani kwa Maendeleo ya Taifa letu”.

Amesema ni lazima Chama Cha Mapinduzi kuendelea kujitambulisha kwa wanyonge na wanaoonewa ili kuwafanya Watanzania kila wanapopata changamoto kufikiria CCM kama mkombozi wa kweli.


Makamu wa Rais amesema wakati Chama hicho kikielekea katika Uchaguzi wa Chama kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa mwaka 2027, ni muhimu sasa wanachama wa CCM kuanza kujiandaa kuelekea huko kwa kuzingatia mambo muhimu na ya msingi ikiwemo kusimamia maadili, umoja na mshikamano wa CCM, Kuendeleza amani na utulivu na kukubali kuwa uongozi ni utumishi wa kutumikia watu.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amekagua maendeleo ya Chuo cha Veta Wilaya ya Chemba, ambapo amepongeza maendeleo ya Chuo hicho kwa kuwa na miundombinu ya kisasa na vifaa vya kisasa vya kujifunzia, vitakavyowasaidia wanafunzi katika kujifunza kwa vitendo hivyo kupata ujuzi utakaoweza kuwasaidia vema.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi, Wabunge pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

05 Februari 2026

Dodoma.




 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI