TAASISI isiyo ya Kiserikali (NGO) Busara Promotions yenye makao makuu yake Unguja, Zanzibar inayoandaa na kuendesha tamasha kubwa la Muziki la Sauti za Busara leo Februari 5, 2026 wametiliana saini Mkataba wa mashirikiano kwa miaka 5 na kampuni ya CPS inayoendesha miradi ya Fumba Town Zanzibar.
Tukio hilo limefanyika mapema leo katika Mkutano wake na vyombo vya habari na wadau mjini Unguja ambapo wamesema kwa pamoja wamepongeza hatua hiyo yenye kuleta mashirikiano na kuongeza fursa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Busara Promotions, Simai Mohamed Said amewashukuru Fumba Town Zanzibar kwa kuendeleza mashirikiano hayo
Aidha, Mkataba huo wa kipindi kingine cha miaka mitano, ikithibitisha upya ushirikiano wa muda mrefu unaolenga kusherehekea urithi wa kitamaduni wa Afrika kupitia muziki na sanaa za ubunifu.
Ahadi hiyo iliyofanyiwa upya inaakisi maono ya pamoja kati ya Fumba Town na Sauti za Busara ya kufungua milango kwa wasanii na vipaji vipya vinavyochipukia, kuwapa jukwaa la kujijengea majina, kukuza mitandao yao, na kuunganishwa kuvuka mipaka ya nchi.
Shughuli za tamasha zitapamba moto kwa burudani mbalimbali zikiwemo muziki, semina jumuishi na mijadala ya kitamaduni, zitakazofanyika katika viunga tofauti vya Zanzibar kuanzia Februari 5-8, 2026.
Sauti za Busara ni jukwaa linalounganisha elimu, sanaa na burudani kwa pamoja.Tamasha hili huwakutanisha watu kutoka mataifa mbalimbali, kila mmoja akiwa na shughuli na utamaduni wake, katika jukwaa moja lililoandaliwa kwa ustadi mkubwa.
Ala za muziki wa asili na wa kisasa hupambwa kwa ladha ya kipekee, zikivuta masikio na mioyo ya wengi na kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha sauti za dunia.
Kwa muda wa siku nne, tamasha hili huwafungulia wakazi wa Unguja fursa lukuki za kiuchumi.
Kuanzia mama ntilie, afisa usafirishaji, wadau wa kazi bunifu hadi wasanii chipukizi, wengi hupata nafasi ya kujitangaza na kujijengea majina kupitia jukwaa hili adhimu.
Mwaka huu, zaidi ya wasanii 400 wa muziki kutoka mataifa 21 wanatarajiwa kutumbuiza Zanzibar. Ni sherehe ya tamaduni, ambapo kila taifa litaleta umahiri wake wa muziki wa asili iwe ni kupitia ngoma, kinubi au zeze.
Tutasherehekea utofauti wetu kupitia majukwaa mawili matatu: Yaani majukwa mawili Mnazi Mmoja na moja Fumba.
Ingawa orodha ya wasanii ni ndefu na ya kuvutia, wengi wameelekeza macho na masikio yao kwa gwiji wa muziki kutoka Mali, Salif Keita. Hata hivyo, atakuwa si peke yake, ataungana na sauti kubwa za Afrika Mashariki akiwemo Ben Pol, pamoja na kinara wa muziki wa Singeli, Man Fongo, kuhakikisha tamasha linabaki kuwa kumbukumbu isiyofutika.
Pamoja na burudani na fursa za kibiashara, Sauti za Busara itaendesha hafua tofauti tofauti zikijadili maswala ya kijamii miongoni ni kuhusu usawa wa kijinsia katika shughuli mbali za kijamii ikiwa ni pamoja na katika muziki. Miongoni mwa mijadala iliyopamba tamasha ni “Inspire to Lead!”, uliofanyika kwa mafanikio makubwa tarehe 17 Januari 2026 katika Viwanja vya Kibanda Maiti.
Mjadala huo ulivutia ushiriki mpana wa jamii na kupokea mrejesho chanya, ukionyesha kiu ya wananchi kushiriki mijadala inayogusa maendeleo ya kijamii.
Mpango huu ni endelevu na utaendelea katika kipindi chote cha tamasha kwa ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Umoja wa Ulaya, pamoja na UN Women.
Kupitia mijadala mbalimbali, wadau hawa wanalenga kuchochea mabadiliko chanya na mapinduzi ya kijamii yanayojikita katika usawa, haki na maendeleo jumuishi.
Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa ni pamoja na kukomesha ukatili dhidi ya wasichana na wanawake, kuhamasisha uongozi wa wanawake, pamoja na kuhimiza utekelezaji wa mipango ya kitaifa kama Tokomeza Vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
Ikiwa ni sehemu ya dhamira yake kwa jamii, Busara Promotions inaripoti mwitikio mkubwa katika mpango wake wa Gender@Work Tanzania, ambao ulipokea jumla ya maombi 179 kutoka nchi 11, ishara ya wazi ya uhitaji na hamasa kubwa katika tasnia ya muziki Afrika.
Mpango huu unalenga kuwajengea uwezo wanawake katika majukumu ya kiufundi na kitaaluma ndani ya tasnia ya muziki, ikiwemo usimamizi wa majukwaa, uzalishaji wa matukio na uratibu wa wasanii, maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakitawaliwa na wanaume.
Ukitekelezwa kwa ushirikiano na Music in Africa Foundation na kufadhiliwa na UNESCO, mradi huu umefanikiwa kuwafunza wanawake 30 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kupitia mpango wa Amplifying Women’s Voices.
Wanufaika wengi sasa wanafanya kazi kama wataalamu hai na wanaotambulika ndani ya sekta ya muziki na burudani.







0 Comments