Na Matukio Daima Media ,Bukoba,Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Ramadhani Kido, Februari 12, 2026 amefika katika Ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera kwa lengo la kusalimia na kujitambulisha rasmi kwa viongozi wa chama ngazi ya Mkoa na Wilaya.
Ziara hiyo imefanyika siku moja baada ya kuwasili mkoani Kagera kufuatia uteuzi wake wa hivi karibuni wa kushika wadhifa huo.
Katika ziara hiyo, Kanali Kido aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Bwana Stephen Ndaki, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mwl. Erasto Sima.
Amepokelewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera (MNEC), Ndugu Kareem Amri, kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa na viongozi wengine wa chama.
Akizungumza katika salamu zake za utambulisho
Kanali Kido amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, kwa kumuamini na kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Amesema ataifanya kazi hiyo kwa uadilifu, bidii na kwa kushirikiana na viongozi wote wa chama na serikali.
Alisisitiza kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano wa dhati katika kutimiza azma ya Rais Dkt. Samia ya kuwahudumia wananchi na kuharakisha maendeleo katika Mkoa wa Kagera.
Kwa upande wake, MNEC wa CCM Mkoa wa Kagera, Ndugu Kareem Amri, alimpongeza Kanali Kido kwa uteuzi huo na kumtakia mafanikio mema katika majukumu yake mapya.
Aidha, alimkabidhi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayobainisha ahadi na mipango ya maendeleo kwa mkoa huo, akimtaka kuisimamia kwa ufanisi kama mtekelezaji mkuu wa serikali mkoani humo.

.jpg)







0 Comments