Na Easter Kameta, UoI
Matukio Daima Media
Wakazi wa mtaa wa Semtema mkoani Iringa wameeleza wasiwasi wao kuhusu kuongezeka kwa uchafuzi wa mazingira unaochangiwa na maji machafu ya mvua, wakisema hali hiyo imekuwa ikisababisha madhara mbalimbali ikiwemo kusambaa kwa taka ovyo na kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko.
Akizungumza na Matukio Daima Media, Goodluck Julius amesema kuwa wakati wa msimu wa mvua, maji yanayosombwa mitaani hubeba taka nyingi kama chupa za plastiki na nepi (pampasi), ambazo husambaa ovyo na kuchafua mazingira.
“Mazingira yanaharibika sana kipindi hiki cha mvua kwa sababu maji husomba chupa za plastiki na taka nyingine na kuzitawanya kila mahali. Hali hii inafanya mitaa ionekane michafu na kuhatarisha afya za wakazi,” amesema Julius.
Naye Raphael Daniel ameeleza kuwa maji yanapotwama katika vidimbwi na mashimo, husababisha harufu mbaya na kuchangia uchafuzi wa hewa. Amesema taka zinazosafirishwa na maji hayo hukwama njiani zinapokutana na vizuizi, jambo linaloongeza uchafu mitaani.
“Maji yanapotwama huleta harufu mbaya, na taka zinazokwama barabarani huharibu taswira ya mazingira yetu,” amesema Daniel.
Kwa upande wake, Rosemarry Mwawa amesema maji machafu yasiyo na mifereji maalum ya kupita yanaweza kusababisha madhara makubwa kiafya, ikiwemo kuenea kwa magonjwa ya mlipuko.
“Maji haya yanapopita ovyo barabarani yanaweza kusababisha magonjwa kama malaria, homa ya matumbo, kichocho na kipindupindu. Ni muhimu jamii kuchukua tahadhari,” amesisitiza Mwawa.
Aidha, Upendo Ezekiel amesema mvua kubwa inaponyesha na maji kupitiliza kwenye mitaro, huweza kuingia mashambani na kuharibu mazao, hali inayosababisha hasara kwa wakulima na kuathiri usafi wa mazingira.
“Mvua kubwa husababisha maji machafu kusambaa na kuharibu mazao pamoja na kuongeza uchafu katika maeneo ya makazi,” amesema Ezekiel.
Wakazi hao wameitaka jamii kuzingatia uchimbaji na uboreshaji wa mitaro ya maji pamoja na utunzaji sahihi wa taka kwa kutumia vyombo maalum, ili kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira na kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
Hatua hizo, kwa mujibu wa wakazi, zitasaidia kulinda afya za wananchi na kuhifadhi mazingira hasa katika kipindi hiki cha msimu wa mvua.

.jpg)






0 Comments