IMEELEZWA kuwa Utulivu na amani ndio nguzo muhimu katika kuchochea maendeleo na ustawi wa jamii kiuchumi.
Rai hiyo imetolewa na Bi. Mosi Mwinyimvua, mkazi wa Mvuti mkoani Dar es Salaam, ambaye amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuendelea kuilinda na kuidumisha amani iliyopo nchini.
Akizungumza nasi leo Jumatano, Februari 11, 2026, Bi. Mwinyimvua amesema kuwa kwa wajasiriamali, hususan wanawake, amani ni msingi wa shughuli zao za kila siku.
“Amani ni kila kitu kwetu. Kama unavyojua sisi akinamama wajasiriamali lazima tutoke kutafuta riziki. Tunasomesha na kulea watoto, na wengine tumeachiwa jukumu hilo peke yetu. Bila amani na utulivu, tutafanyaje kazi? Watoto wetu wataishije? Amani ni muhimu sana,” amesema Bi. Mwinyimvua.
Ameeleza kuwa kukosekana kwa amani huathiri moja kwa moja shughuli za kiuchumi na kijamii, na kusababisha hofu pamoja na kuporomoka kwa kipato cha wananchi. Hivyo, ametoa wito kwa kila Mtanzania kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuimarisha amani kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa mujibu wa tafiti na maandiko mbalimbali, amani huchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni kwa kuwa huwapa wananchi uhuru na mazingira salama ya kutekeleza shughuli zao za kila siku bila wasiwasi. Hali hiyo hutajwa kuwa chachu ya mafanikio na ustawi wa jamii yoyote, huku manufaa yake yakionekana katika nyanja zote za maisha ya binadamu.






0 Comments