Header Ads Widget

WATUMISHI RAS KIGOMA WABANWA KUZINGATIA MAADILI



Na Fadhili Abdallah,Kigoma

Watumishi wa umma kutoka ofisi ya Katibu Tawala (RAS)  mkoa Kigoma wametakiwa kuzingatia misingi mikuu mitatu ya sheria ya  maadili ili kuwezesha kutekeleza majukumu yao kwa tija.

Afisa Habari Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa Umma, Rocky Setembo alisema hayo akitoa mafunzo ya siku moja kwa watendaji wa ofisi ya RAS mkoa wa  Kigoma na kubainisha kuwa misingi hiyo mitatu ya maadili inatija kubwa katika kuhakikisha watumishi wanatimiza majukumu yao.

Setembo alisema kuwa vinginevyo mtumishi ambaye hatatimiza misingi hiyo atakuwa anafanya kazi akiwa na changamoto kubwa za kiutendaji. 


Aliitaja misingi hiyo kuwa Mtumishi kuwa na taaluma na kufanya kazi kwa weledi kwakutumia taaluma yake, mtumishi kuwa mwaminifu kwa kila jambo analolifanya lakini pia utendaji wake uzingatie maslahi ya umma na kuwajibika kwa umma na kwamba misingi hiyo mitatu inapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta tija kwenye utendaji kwa watumishi hao.

Akizungumza katika mafunzo hayo ya siku moja Mhasibu Mkuu ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma, Johson Gamba aliwataka watumishi hao kuzingatia sheria mbalimbali za utumishi ambazo ndiyo dira na mwongozo wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.


Gamba aliwakumbusha watumishi hao kuwasilisha serikalini zawadi wanazopewa wanapotekeleza majukumu yao kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa Kigoma ili zawadi hizo ziingie kwenye rekodi za serikali na kukatiwa risiti ili zisihesabike kama rushwa kwa watumishi.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Huduma za usimamizi, ufuatiliaji na ukaguzi ofisi ya RAS Kigoma, Dorothe Japhet alisema kuwa mafunzo hayo siyo mapya kwao lakini yanawakumbusha kuyatekeleza kwa vitendo kwani ndiyo msingi wa utendaji wao lakini baadhi ya watumishi wamekuwa wakifanya kazi bila kuzingatia sheria na taratili hizo za maadili ya utumishi.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI