Serikali ya Uganda imetangaza kufunguliwa tena kwa mitandao ya kijamii baada ya kuminywa kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika mapema mwezi Januari.
Siku ya Jumatatu, Januari 26, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda (CDF), Jenerali Muhoozi Kainerubaga, alitangaza kuondolewa kwa marufuku ya kuminya majukwaa ya mitandao ya kijamii, akiwashukuru Waganda kwa ushirikiano wao katika kipindi chote cha uchaguzi.
Katika taarifa hiyo, Muhoozi aliwasifu Waganda kama watu bora zaidi duniani. Pia alibainisha kuwa uungwaji mkono alioupata kutoka kwa Waganda ulimpa yeye na timu yake ujasiri wa kutumikia, na kuombea baraka nchi na raia wake.
"Tunaachilia mitandao yote ya kijamii leo. Ninawashukuru raia wote wa Uganda kwa ushirikiano wao katika msimu huu wote wa uchaguzi," Muhoozi alisema.
"Ninyi ni watu bora zaidi duniani, na mnatupa ujasiri wa kutumikia. Mungu awabariki nyote," aliongeza.
Kabla ya uchaguzi, serikali ya Uganda ilitangaza kufungwa kwa intaneti kote nchini ambako kuliathiri huduma zote za simu na setilaiti, ikitaja hitaji la kupunguza ukiukwaji wa sheria za uchaguzi na kulinda utulivu wa umma wakati wa kipindi cha uchaguzi.
Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC), mnamo Januari 18, iliondoa marufuku ya mtandao lakini ikaagiza kwamba mitandao ya kijamii na programu za ziada (OTT) ziendelee kuzuiwa hadi itakapotangazwa tena.
Kulingana na tume hiyo, majukwaa kadhaa ya mitandao ya kijamii yalisalia kuwekewa vikwazo. Programu hizo ni pamoja na WhatsApp, TikTok, X (zamani Twitter), Instagram, Telegram na app stores, huku Facebook ikiendelea kusimamishwa tangu 2021.





0 Comments