Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imesajili jumla ya wafanyabiashara ndogondogo 119,595 katika Mfumo wa Usimamizi na Usajili wa Wafanyabiashara Ndogondogo (WBNMIS), hatua inayolenga kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kunufaika na fursa mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa wizara hiyo, Mheshimiwa Dorothy Gwajima, amesema mafanikio hayo yamepatikana katika kipindi cha siku 100 za utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo Serikali imejikita katika urasimishaji wa wafanyabiashara, utoaji wa mikopo nafuu na uwezeshaji wa makundi maalum.
"Kati ya waliosajiliwa wanawake ni 73,341 na wanaume 46,254, huku makundi yaliyosajiliwa yakijumuisha machinga 103,102, mama na baba lishe 12,384 pamoja na waendesha bodaboda na bajaji 4,109," Amesema Waziri Gwajima.
Ameeleza kuwa katika kipindi hicho, Serikali imepokea Shilingi bilioni 10.5 kwa ajili ya kutoa mikopo yenye masharti nafuu na riba ya asilimia saba kwa mwaka kwa wafanyabiashara ndogondogo, ambapo Shilingi bilioni 1.35 tayari zimetolewa kwa wafanyabiashara 588 kupitia Benki ya NMB, na zoezi la utoaji mikopo linaendelea kote nchini.
Aidha, amesema kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Shilingi milioni 337.9 zimetolewa kwa wanawake wajasiriamali 45 kwa riba ya asilimia nne, huku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikirasimisha waendesha pikipiki na bajaji 209,632 kwa kuwapatia leseni za udereva.
Kwa upande wa vikundi vya wajasiriamali, Waziri Gwajima amesema jumla ya vikundi 6,041 vimetambuliwa na kusajiliwa kupitia mfumo wa Wezesha Portal, na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 33 imetolewa kwa vikundi 3,776 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akizungumzia dhamira ya Serikali, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kwa vitendo kuhakikisha inatekeleza kikamilifu ahadi zake kwa wananchi, akisisitiza kuwa utekelezaji huo unaonekana wazi kupitia miradi na mipango mbalimbali inayotekelezwa katika sekta tofauti.
Msigwa ameongeza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kusimamia maendeleo jumuishi yanayogusa makundi yote ya jamii, huku akiitaka jamii kushiriki katika kumbukizi ya Rais Samia kwa kuchukua hatua za vitendo za kulinda mazingira.
Amehimiza wananchi katika maeneo yao kupanda angalau mti mmoja kama ishara ya kumuunga mkono Rais Samia katika juhudi za utunzaji wa mazingira na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.










0 Comments