Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, leo Januari 09, 2026 yuko mkoani Arusha akimuwakilisha Waziri wa afya Mhe Mohamed Mchengerwa kwa ziara ya kikazi yenye lengo kufunga kambi maalum ya matibabu ya moyo na kufuatilia uimarishaji na utekelezaji wa huduma za kibingwa na kibingwa bobezi za magonjwa ya moyo kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kusogeza huduma maalum za afya karibu na wananchi wa Kanda ya Kaskazini.
Akiwa mkoani humo, Dkt. Samizi amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Amos Makalla, ambapo wamejadili kwa kina uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika sekta ya afya mkoani Arusha, hususan katika uboreshaji wa miundombinu ya hospitali, upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa na ongezeko la wataalamu wa afya.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Samizi ameeleza kuwa uwekezaji huo umeongeza uwezo wa Mkoa wa Arusha kutoa huduma bora za afya kwa wananchi na wageni, na kwamba utaendelea kurahisisha mahitaji ya huduma za matibabu wakati wa mashindano makubwa ya AFCON 2027, ambapo Mkoa wa Arusha unatarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya shughuli za mashindano hayo.
Aidha, viongozi hao wamewapongeza watumishi wa sekta ya afya mkoani Arusha kwa kazi kubwa na ya kujitolea wanayoendelea kuifanya, wakisisitiza kuwa mchango wao ni nguzo muhimu katika kufanikisha azma ya Serikali ya kuboresha huduma za afya, kuimarisha mifumo ya rufaa na kuiweka Arusha katika hadhi ya kimataifa kwa huduma za afya na utalii wa tiba.











0 Comments