Wananchi wanufaika kielimu na kiuchumi
Januari 10, 2026 , Shughuli za uchukuaji miche ya miti zinaendelea kwa ufanisi katika bustani za miche zilizopo Tarafa ya Kwanza Irundi na Tarafa ya Tatu Ihalimba ndani ya Shamba la Miti Sao Hill, ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa upandaji miti Shamba la Miti Sao Hill kwa lengo la kuendeleza misitu ya kupandwa ili kuongeza uzalishaji wa rasilimali za misitu na kuhakikisha uendelevu wa uhifadhi wa mazingira.
Katika zoezi hilo, wananchi kutoka maeneo yanayozunguka Shamba la Miti Sao Hill wamepata fursa ya kushiriki kikamilifu, hali iliyowezesha kupatikana kwa ajira za muda na hivyo kuongeza kipato chao na kuboresha maisha yao ya kila siku.
Mbali na kunufaika kiuchumi, wananchi wanaoshiriki zoezi hilo wamepata elimu ya vitendo kuhusu namna bora ya kuandaa na kusimamia bustani za miche ya miti, kuanzia hatua za upandaji wa mbegu, utunzaji wa miche hadi maandalizi ya miche kwa ajili ya kupandwa shambani.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Said Singano, alisema kuwa uchukuaji wa miche unafanyika kwa kuzingatia taratibu na kanuni za kitaalamu ili kuhakikisha miche inabaki na ubora unaohitajika.
“Tunasisitiza miche ichukuliwe kwa uangalifu mkubwa ili isiharibu mizizi, kwa sababu ubora wa miche ndiyo msingi wa mafanikio ya upandaji mashambani,” alisema Singano.
Vilevile, kupitia zoezi hilo, wananchi hao wamejifunza kwa vitendo kuhusu mbinu bora za upandaji miti mashambani, ikiwemo nafasi sahihi kati ya mti na mti, muda unaofaa wa kupanda, pamoja na matunzo ya awali baada ya upandaji.
Shughuli hizi pia zimeongeza uelewa wa wananchi kuhusu mchango wa Shamba la Miti Sao Hill katika uhifadhi wa mazingira, kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa mazao ya misitu kwa manufaa ya Taifa.
Mmoja wa wananchi aliyeshiriki zoezi la upandaji miti, Bw. Joshua Ng'umbi kutoka Kijiji cha Igowole Wilayani Mufindi, alisema kuwa kushiriki shughuli hizo kumemsaidia kuongeza kipato pamoja na kupata ujuzi mpya wa shughuli mbalimbali za upandaji miti na uhifadhi wa misitu.
“Mbali na kupata ajira, nimejifunza jinsi ya kuchagua miche bora na namna sahihi ya kupanda miti ili iweze kuota vizuri kwani miti hii inatakiwa ikue vyema ili inavunwa iwe na ubora mzuri ambao utasababisha kupata pesa nyingi,” alisema Bw Joshua
Kwa ujumla, zoezi la uchukuaji miche katika Tarafa za Irundi na Ihalimba limeendelea kuwa na manufaa makubwa kwa Shamba la Miti Sao Hill na wananchi wanaoshiriki, kwa kuimarisha juhudi za upandaji miti mashambani, kutoa ajira na kukuza uelewa na ujuzi wa masuala ya misitu na uhifadhi wa mazingira.










0 Comments