Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
HALI ya utulivu iliyopo mkoani Morogoro imetajwa kuwa ni matokeo ya ushirikiano kati ya wananchi, viongozi wa dini na Serikali katika kulinda amani ya Taifa.
Aidha waumini wa dini ya Kiislamu Mkoa wa Morogoro wamepongezwa kwa kuendelea kudumisha utulivu, umoja na mshikamano licha ya nchi kupitia changamoto za kisiasa zilizoambatana na matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoripotiwa Oktoba 29 katika baadhi ya maeneo nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala akitoa salamu za Serikali katika hafla ya Iftar iliyoambatana na Dua ya kuliombea Taifa na kuwakutanisha waumini, viongozi wa dini na Serikali.
Alisema wananchi wa Morogoro wanapaswa kuendelea kuwa walinzi wa kwanza wa amani kwa kuimarisha mshikamano huo, uvumilivu na kuheshimiana katika jamii.
Alisema utulivu wa Mkoa wa huo ni mfano wa kuigwa kwa maeneo mengine nchini, huku akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kuitunza na kuilinda.
Kilalaka pia alizungumzia suala la miradi ya Maendeleo iliyopo ndani ya Wilaya ya Morogoro ambapo alitolea mfano mradi wa standi ya kisasa ya daladala inayojengwa pembeni ya kituo cha SGR cha Morogoro Cha Jakaya Kikwete ambayo Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 13.
"Miradi kadhaa ya Maendeleo inaendelea wilayani hapa na utekelezaji wake umelenga kuboresha huduma muhimu za kijamii kwa kuchochea ukuaji wa uchumi,"alisema.
Aliitaka baadhi ya miradi ni pamoja na barabara ya Bigwa - Kisaki ambayo itakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha shughuli za kiuchumi, pamoja na sekta ya kilimo na afya.
Alieleza kuwa katika Halmashauri mbili za Wilaya hiyo ya Morogoro hali ya upatikanaji wa huduma za matibabu zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake, Mwanazuoni na Mhadhiri wa Kimataifa wa Dini ya Kiislamu ambaye alikuwa mgeni maalumu, Sheikh Rashid Mziwanda alisema ni muhimu kwa viongozi wa dini kutumia majukwaa yao kuhubiri amani, upendo na mshikamano ili kuimarisha utulivu wa Taifa.
"Tumieni majukwaamkama haya kuwaunganisha watu katika kuleta Amani na upendo, ni jambo la aibu kuwaona viongozi wa dini wanakuwa mstari wa mbele kuchochea vurugu,"alisema.
Aidha, Sheikh Mziwanda alitoa onyo kwa baadhi ya viongozi wa dini wanaojihusisha na matamko yanayoweza kuiingiza nchi katika hali ya taharuki, akiwataka kutanguliza busara na kutumia nafasi zao kuunganisha jamii badala ya kuibua migawanyiko.


.jpg)



.jpg)




0 Comments