Header Ads Widget

PROFESA JANABI ATAKA HUDUMA RAFIKI SEKTA YA AFYA

NA MWANDISI WETU, DAR

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi anasema mapambano dhidi ya Ukimwi hayawezi kufanikiwa bila kuwafikia watu wote, hasa makundi yaliyo hatarini. 

Akihutubia kwenye mkutano wa Kimataifa wa Ukimwi na magonjwa ya zinaa Afrika (ICASA) uliofanyika Accra Ghana hivi karibuni, Profesa Janabi anashauri huduma za afya ziwe rafiki, salama na zisizo na ubaguzi.

Katika ujumbe wake kwa ICASA, Profesa Janabi anasema makundi muhimu katika vita dhidi ya Ukimwi ni pamoja na mashirika ya kijamii na haki za binadamu akiyataja kuwa ni washirika muhimu na ni msingi wa afya bora huku akizitaka Serikali kuimarisha mifumo ya afya na kuongeza bajeti zake.

“Tuhakikishe hakuna anayeachwa nyuma katika mapambano hayo, mapambano dhidi ya Ukimwi hayawezi kufanikiwa bila kuwafikia watu wote, hususan makundi yaliyo hatarini zaidi, vijana na wasichana pamoja na jamii zinazokumbwa na unyanyapaa na ubaguzi, hivyo huduma za afya zinapaswa kuwa rafiki, salama na zisizo na ubaguzi”alisisitiza.

Aidha mkurugenzi huyo wa WHO Kanda ya Afrika, alishauri huduma za vvu ziunganishwe na afya kwa ujumla ikiwemo huduma za afya ya msingi, bima ya afya (UHC), huduma za afya ya uzazi akisema hiyo itasaidia watu kupata huduma kwa urahisi na kwa muda mrefu hata baada ya misaada ya wafadhili kuisha.

Kwa upande wake, Mtaalam wa masuala kijamii, Atupakisye Mwaifunga wa taasisi ya Tusemezane ya jijini Dar es Salaam anasema unyanyapaa kwa makundi maalum una athari kubwa kiafya, kijamii na kiuchumi.

Anasema mtu aliyenyanyapaliwa au kubaguliwa kutokana hali yake ya kimwili, kihisia hujenga hofu, aibu na kujitenga na jamii na mwishowe huathirika kisaikolojia na hatimaye uchumi wake huyumba.

Mwaifunga anasema katika sekta ya afya, unyanyapaa huathiri moja kwa moja upatikanaji wa huduma, ambapo makundi haya mara nyingi huchelewa au huacha kabisa kufuata matibabu kwa sababu ya kauli za dharau, ubaguzi au kukosa usiri katika vituo vya kutolea huduma.

“Hali hii huongeza hatari ya maambukizi mapya, kuenea kwa magonjwa na vifo vinavyoweza kuzuilika, huku ikidhoofisha juhudi za afya ya umma.

“Unyanyapaa humjengea mtu huyo hofu, hali inayowafanya watu hawa kuficha utambulisho au hali zao halisi ili kuepuka kubaguliwa. Matokeo yake, wengi hushindwa kushiriki kikamilifu katika masuala ya jamii au kupata huduma muhimu kwa hofu ya kunyanyaswa au kudhalilishwa.

“Kisaikolojia, unyanyapaa huongeza msongo wa mawazo, mfadhaiko na matatizo ya afya ya akili. Kukataliwa na familia au jamii huyafanya makundi haya ya watu kujiona hawana thamani, hali inayoweza kusababisha matumizi ya dawa za kulevya, ulevi kupindukia, vitendo vya kujiumiza au kuishi maisha ya hatari. Kwa makundi haya, ukosefu wa ulinzi wa kijamii huongeza ukatili kwa namna moja au nyingine”anasisitiza Mwaifunga.

Dkt Johnmary Laurian wa Bunju Dar es Salaam anauelezea unyanyapaa kuwa ni suala mtambuka lenye athari kubwa kwa jamii.

Anasema makundi yanayobaguliwa kutokana na hali zao za kiafya na maumbile huwasababisha kushindwa kupata ajira rasmi, elimu au hata makazi salama. Na kwamba wanapojitenga au kutengwa na familia na jamii, wanakuwa katika mazingira hatarishi zaidi jambo linalowazuia kutoka katika maisha ya utegemezi au hatari.

“Kwa mfano, binti aliyepata mimba za utotoni na kujifungua mapema, au mtu anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja anaweza kufukuzwa nyumbani na kulazimika kuingia katika biashara ya ngono.

“Unyanyapaa huathiri afya ya akili ya watu wanaolengwa, watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja au wanaofanya kazi ya kuuza mili yao, mara nyingi hukumbwa na msongo wa mawazo, huzuni, au hata kujiua kutokana na kutengwa, kubezwa au kudhalilishwa na jamii.

“Hofu ya kuhukumiwa huwafanya wajifiche au kushindwa kujiamini, hivyo kuathiri uwezo wao wa kutafuta msaada wa afya au msaada wa kijamii.”anasema Dkt Laulian

Tanzania kupitia mpango wa kitaifa wa kudhibiti vvu, magonjwa ya zinaa na ini (NASHCOP) imeweka miongozo rasmi ya kupambana na unyanyapaa na ubaguzi hasa katika sekta ya afya. Hii ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha huduma za afya zinapatikana bila ubaguzi.

Pia kupitia sera na sheria za haki za binadamu na utoaji wa huduma zenye ulinzi na usawa, serikali imeweka msisitizo wa kutekeleza sheria zinazopinga ubaguzi na vitendo vya kibaguzi dhidi ya watu kwa misingi mbalimbali ikiwemo hali ya afya. Hii ni pamoja na utekelezaji imara wa sheria za kitaifa ambazo zinaimarisha msimamo wa kutokubali ubaguzi na unyanyapaa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI