Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kwa kushirikiana na Shirika la ADAP (_Association for the Development of Protected Areas_) imeongoza hatua za uanzishwaji wa Jukwaa la Wadau wa Uyoga nchini, hatua itakayowezesha wadau wa Sekta ya Uyoga kunufaika kiuchumi na kuongeza kipato kupitia maendeleo ya zao hilo.
Akizungumza leo Machi 13, 2026 katika Makao Makuu ya TAFORI, Morogoro, wakati wa mkutano wa Uanzishwaji wa Jukwaa la Wadau wa Uyoga Tanzania, Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt. Revocatus Mushumbusi, alisema jukwaa hilo litaratibu juhudi za Wadau wa Sekta ya Uyoga nchini kwa kuwawezesha kubadilishana maarifa na uzoefu pamoja na kuendeleza sekta hiyo.
Alisema kuanzishwa kwa jukwaa hilo kunalenga kuchangia maendeleo ya ustawi wa uhifadhi wa misitu, uchumi wa wananchi na kuongeza mchango wa zao hili katika pato la Taifa.
Aidha, alisema jukwaa hili litakuwa chombo muhimu cha kutoa ushauri wa kisera, kuhamasisha uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa Kitaifa na Kimataifa.
“Ni matumaini yangu kuwa kupitia chombo hiki, Wadau wataibua mawazo mapya, kuimarisha ushirikiano na kuweka mikakati madhubuti itakayosaidia kuendeleza Sekta ya Uyoga, usalama wa chakula, maendeleo ya uchumi yanayoweza kumgusa Mwananchi moja kwa moja na uhifadhi wa mazingira,” alisema.
Dkt. Mushumbusi alisisitiza ni muhimu kuimarisha tafiti za Kisayansi kuhusu aina na thamani ya uyoga ili zao hili liweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa Taifa. Aliongeza kuwa hatua hiyo iende sambamba na kujenga uwezo wa jamii katika kutambua uyoga unaoliwa na wenye sumu, pamoja na kuendeleza teknolojia za uongezaji thamani na kuimarisha masoko ya bidhaa za uyoga.
Alisema uyoga una mchango katika utekelezaji wa Sera mbalimbali za Taifa, ikiwemo Sera za Taifa za Kilimo na Lishe kwa kuongeza upatikanaji wa chakula chenye virutubisho muhimu. Pia alieleza kuwa maendeleo ya zao hilo yanaweza kuchochea ukuaji wa viwanda vidogo na vya kati kupitia uongezaji thamani kama ukaushaji, usindikaji na ufungashaji wa uyoga, hali itakayosaidia kuongeza ajira na kipato kwa Wananachi na hasa makundi maalumu ya kijamii wakiwepo Wanawake na Vijana.
Hatua ya kuanzishwa kwa Jukwaa la Uyoga nchini imefuata baada ya kufanyika kwa Warsha ya Wadau wa Uyoga iliyofanyika Mkoa wa Tabora mwezi Februari, 2025.
Mkutano huo umehudhuriwa na Wadau mbalimbali kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Wizara ya Mambo ya Ndani, Meneja wa Shirika la ADAP, Mshauri wa Uyoga na Uhifadhi wa Misitu wa Shirika la ADAP, pamoja na Wakusanyaji na Wafanyabiashara wa Uyoga.

.jpg)


.jpg)




0 Comments