Meneja wa Lushoto Executive Lodge, Bw. Sifa Mwambire, amewakaribisha wageni wa ndani na nje ya nchi kutembelea wilaya ya Lushoto na kufurahia huduma bora pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana katika eneo hilo lenye mandhari ya kipekee.
Akizungumza hivi karibuni, Bw. Mwambire alisema kuwa Lushoto Executive Lodge imejipambanua kwa kutoa huduma za kiwango cha juu katika mazingira tulivu na salama, huku ikilenga kuwahakikishia wageni faraja, ukarimu na mapumziko yenye ubora. Alisema lodge hiyo ni mahali sahihi kwa wageni wanaotafuta utulivu na huduma bora za malazi.
Bw. Mwambire, ambaye pia ni mmoja wa wadau na wadhamini wakubwa wa walkathon iliyofanyika Magamba wilayani Lushoto, alisema ushiriki wao katika kudhamini tukio hilo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kukuza utalii na kuhamasisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika wilaya hiyo.
Alibainisha kuwa Lushoto imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ikiwemo milima ya Usambara, misitu ya asili, maporomoko ya maji, maeneo ya kihistoria na mandhari ya kuvutia ambayo huwafanya wageni kufurahia safari zao.Kwa mujibu wake, vivutio hivyo vina mchango mkubwa katika kuitangaza Lushoto kama kitovu cha utalii wa ikolojia.
Akizungumzia hali ya hewa, Meneja huyo alisema Lushoto ina hali ya hewa ya baridi na ya kupendeza kwa kipindi chote cha mwaka, hali inayowavutia wageni wengi wanaotaka kupumzika mbali na joto kali la miji mingine. Aliongeza kuwa mazingira ya kijani kibichi ya mji huo huongeza mvuto wa kipekee kwa wageni.
Mwisho, Bw. Sifa Mwambire aliwataka wadau wa utalii, wananchi na wageni kushirikiana kuitangaza Lushoto kama moja ya maeneo bora ya utalii nchini.Alisisitiza kuwa Lushoto Executive Lodge itaendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiutalii kwa lengo la kuunga mkono maendeleo endelevu ya wilaya hiyo.






0 Comments