Header Ads Widget

WENYE ULEMAVU WAANDIKA HISTORIA MPYA KUPITIA MASHINDANO YA QUR’AN DODOMA

 


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

Katika taswira mpya ya kuongeza ushiriki na kuthibitisha uwezo wa watu wenye ulemavu, jiji la Dodoma leo limekuwa kitovu cha historia ya kipekee baada ya kuzinduliwa msimu wa pili wa mashindano ya kusoma Qur’an Tukufu kwa watu wenye ulemavu, mashindano yanayotajwa kuwa ya kwanza duniani kwa aina yake. 

Tukio hilo limeibua hisia za matumaini, uthubutu na msukumo mpya wa kuthibitisha kuwa ulemavu si kikwazo cha vipaji wala imani.


Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Ummy Ndeliananga ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum kwa watu wenye ulemavu, amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa nguzo muhimu katika kuimarisha ustawi wa watu wenye ulemavu nchini. 

Amesema Rais Samia ameendelea kusimama bega kwa bega na kundi hilo kwa kuhakikisha wanapata amani, heshima na nafasi sawa katika jamii, jambo linaloleta tabasamu na kuondoa ukinzani wa kijamii uliokuwepo hapo awali.


Katika uzinduzi huo, Mwanzilishoi wa mashindano hayo na Mkurugenzi wa Riziki Rurida Foundation na Mwenyekiti wa Sauti ya Wenye Ulemavu na kiongozi Wanawake Wenye Ulemavu, Riziki Saidi Rurida, ameeleza kuwa wazo la mashindano hayo limetokana na hamasa aliyoipata kupitia mikutano ya kimataifa ya watu wenye ulemavu pamoja na safari yake ya hija mjini Makka ambako alipata huduma za kipekee zilizoamsha ndani yake ari ya kuwainua watu wenye ulemavu.

 Amesema ulemavu wake ulitokana na ajali, lakini hilo halikumzuia kusimama imara na kufanikisha mashindano ambayo mwaka jana yaliwezesha baadhi ya washindi kupata pikipiki na bajaji kama motisha ya kuendeleza maisha yao. 

Amesisitiza kuwa Tanzania imeweka rekodi kwa kuwa nchi ya kwanza duniani kuandaa mashindano ya Qur’an kwa watu wenye ulemavu, huku akiwahimiza wazazi kuacha ubaguzi hasa katika ndoa, kwani upendo ndio msingi mkuu na hata kiimani kitendo hicho kina baraka.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Afisa Maendeleo ya Jamii Hidaya Abdallah amesema mashindano hayo ni chachu ya kuongeza maarifa, kuimarisha usomaji wa Qur’an na kujenga jamii yenye heshima na uelewa mpana kuhusu haki za watu wenye ulemavu. 

Amesema umuhimu wake unapaswa kusambaa katika makundi yote ya rika ili kujenga taifa linalotambua thamani ya ushirikishwaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation for Disabilities Hope (FDH),Maiko Salali, amesema mashindano hayo yamekuwa daraja linalounganisha watu wenye ulemavu kutoka mikoa mbalimbali na kuwawezesha kuonesha vipaji vyao mbele ya jamii.

 Amesema lengo ni kuyaendeleza katika ngazi ya kitaifa na baadaye kimataifa, huku akiwasihi watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kwani fursa na zawadi ni nyingi.

Mwakilishi wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Dodoma, Hussein Ngula, amesema msimu huu wa mashindano umeongeza ari na kuimarisha imani ya watu wenye ulemavu kwamba wanathaminiwa kama watu wengine. 

Amesema maamuzi yanayowaleta pamoja bila ubaguzi na kumtegemea Mungu ndiyo msingi wa kuendelea kujenga jamii inayoheshimu utu wa kila mtu.


Ikiwa mashindano haya yataendelezwa hadi ngazi ya kimataifa kama ilivyopendekezwa, Tanzania inatajwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuunganisha imani, vipaji na ujumuishi kwa manufaa ya watu wote.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI