Na Fadhili Abdallah,Kigoma
POLISI mkoa Kigoma kwa kushirikiana na jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) wameanza doria ya pamoja ya kudhibiti vitendo vya uhalifu na uporaji wa zana za uvuvi vinavyofanywa kwenye mwambao wa ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.
Mkuu wa wilaya Uvinza, Dinnah Mathamani amezindua zoezi hilo kwenye mwalo wa Muyobozi kijiji cha Mwakizega wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ikiwa ni kutekeleza agizo la Mkuu wa mkoa Kigoma, Balozi Simon alilolitoa juzi katika kijiji cha Lubengera wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Kuanza kwa doria hiyo ya pamoja kunakuja baada ya malalamiko ya wavuvi na wachakataji wa mazao ya uvuvi kulalamika kuwepo kwa matukio ya mara kwa mara ya wizi za zana za uvuvi unaofanywa na wahalifu wanaosadikiwa kutoka jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Akizundua zoezi hilo Mkuu huyo wa wilaya Uvinza alisema kuwa pamoja na kufanyika kwa doria hiyo pia vyombo vingine vya ulinzi na usalama ikiwemo idara ya uhamiaji vitaendelea na majukumu yake ikiwemo kukagua watu wote wanaoishi na kufanya kazi kwenye vijiji vya mwambao wa ziwa Tanganyika na watakaobainika kuishi bila kufuata taratibu watachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Uvinza, Fred Millanzi alisema kuwa Halmashauri hiyo inazo boti tano ambazo zitatolewa kusaidia jukumu hilo zikigawanywa kulingana na maeneo ya kiutendaji yatakayoelekezwa.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi huo akiwemo Zuberi Haruna mvuvi katika mwalo wa Muyobozi kijiji cha Mwakizega amesihukuru serikali hususani Mkuu wa mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro kwa hatua za kurudisha doria ya pamoja na polisi na jeshi la wananchi kwani hali ya ujambazi ziwa Tanganyika ilifikia kwenye hatua mbaya na wavuvi waliingia woga kununua vifaa vya thamani kuimarisha shughuli zao.









0 Comments