Rungwe. Hifadhi ya Mazingira Asilia Mlima Rungwe imeanza kampeni maalumu ya kuwajengea uelewa wanamitindo kuhusu umuhimu wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika eneo hilo, hususan Ziwa Ngosi, ambalo linatarajiwa kuwa moja ya maeneo muhimu ya shughuli za kinyang’anyiro cha Mr & Miss Mt Rungwe pamoja na tukio la utalii la “Tukutane Mount Rungwe – Season II.”
Tukio hilo linaandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na kampuni ya Tanzanite Legacy Sports & Adventure, likiwa na lengo la kukuza utalii wa mazingira, kuhamasisha vijana kuthamini rasilimali za asili na kuitangaza kimataifa Hifadhi ya Mazingira Asilia Mlima Rungwe.
Akizungumza wakati wa shughuli ya utambulisho wa kivutio hicho, Machi 14,2026, Mkuu wa Safu ya Poroto, Mhifadhi Ridhiwani Gambalela amesema Ziwa Ngosi ni miongoni mwa maeneo ya kipekee yenye uzuri wa asili na mandhari inayovutia, hali inayolifanya kuwa kivutio muhimu katika kukuza utalii wa ndani na wa kimataifa.
Amesema ziwa hilo lina mazingira tulivu yaliyozungukwa na kijani kibichi cha milima ya Poroto, hali inayowapa wageni fursa ya kufurahia hewa safi ya milimani, kusikiliza sauti za ndege wa porini na kushuhudia uzuri wa mazingira ambayo bado hayajaathiriwa sana na shughuli za kibinadamu.
Mbali na uzuri wake wa asili, Gambalela amesema Ziwa Ngosi lina historia na simulizi za kipekee za eneo hilo, jambo linalolifanya kuwa kivutio kinachoweza kuwavutia wageni wanaopenda kujifunza kuhusu mazingira na tamaduni za wenyeji.
Kwa mujibu wa Gambalela, washiriki wa shindano la Mr & Miss Mt Rungwe wanatarajiwa kutumia mandhari ya ziwa hilo katika shughuli mbalimbali za utangazaji, ikiwamo upigaji picha za utalii na kampeni za kuhamasisha vijana kushiriki katika kulinda na kutangaza vivutio vya asili.
Katika tukio hilo la Tukutane Mount Rungwe – Season II, washiriki na watalii watapata fursa ya kushiriki shughuli mbalimbali za utalii wa asili ikiwamo hiking na trekking, bird watching, nature walk, camping, yoga na meditation pamoja na burudani ya karaoke, shughuli zinazolenga kuwapa wageni uzoefu wa karibu na mazingira ya mlima Rungwe.
Kwa mujibu wa waandaaji, Tanzanite Legacy kupitia Mkurugenzi wake Bi Hellen Stima tukio hilo litafanyika kwa siku mbili ambapo tarehe 27 Machi 2026 kutakuwa na shughuli za camping kwa gharama ya Sh50,000, huku tarehe 28 Machi 2026 kukiwa na ziara ya siku moja (day trip) kwa gharama ya Sh20,000 kwa mshiriki.
Bi Hellen Stima amewahamasisha wananchi, watalii wa ndani na nje ya nchi pamoja na wapenzi wa utalii wa mazingira kushiriki tukio hilo ili kujionea uzuri wa Mlima Rungwe na Ziwa Ngosi.
Aliongeza kuwa wanaotaka kushiriki, waandaaji wamewataka kufanya uhifadhi (booking) mapema kupitia namba +255 757 677 704 au +255 672 800 124 ili kupata nafasi ya kushiriki safari hiyo ya kipekee ya utalii wa asili katika milima ya Kusini mwa Tanzania.











0 Comments