Header Ads Widget

DIWANI MTEULE CCM AFARIKI KWA MADAI YA KUNYWA MAJI YA BETRI



Lusekelo Mwalukomo enzi za uhai wake
 

Na Moses Ng’wat, Mbozi.

DIWANI mteule wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Shiwinga, Wilaya ya Mbozi, Lusekelo Mwalukomo, amefariki dunia baada ya kudaiwa kunywa maji ya betri, tukio lililotokea Novemba 26, 2025 wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mbozi Mission.

Taarifa za awali kutoka kwa ndugu wa karibu na baadae kuthibitishwa na baba yake, Mchungaji mstaafu Ambukege Mwasomola, zinaeleza kuwa diwani huyo alikimbizwa hospitalini baada ya kunywa maji ya betri ya solar yaliyokuwepo nyumbani kwake, siku chache baada ya kurejea nyumbani akitokea hospitali alikokuwa amelazwa kwa siku kadhaa kutokana na kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya tukio hilo, alisema hakuna taarifa yoyote ya tukio hilo iliyoripotiwa polisi.

“Sijaipokea taarifa hiyo, kama kweli angekunywa maji ya betri, kwa taratibu zilivyo lazima ingeripotiwa polisi ili kutolewa fomu kwa ajili ya matibabu... ntaendelea kufuatilia, tukipata taarifa kamili tutaeleza,” alisema Kamanda Senga.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, amethibitisha kifo hicho na kusema sababu za diwani huyo kunywa maji ya betri bado hazijajulikana, ingawa taarifa za awali zinadai huenda lilihusishwa na msongo wa mawazo.

“Wataalamu wanaendelea kuchunguza kubaini chanzo kamili, marehemu alikunywa maji ya betri asubuhi ya Novemba 26, 2025, na madaktari walijitahidi kumwokoa bila mafanikio,” alisema DC Mbega.

Akizungumza kutoka kijijini Shiwinga, baba wa marehemu Mchungaji Mwasomola, alisema mwanawe alianza kuugua wakati wa michakato ya uchaguzi  Mkuu wa Oktoba 29, 2025, na mara kadhaa alilalamikia kuishiwa nguvu na kukosa hamu ya kula.

Alisema marehemu mwenyewe alimueleza mkewe kuwa amekunywa maji ya betri alipokuwa ametoka kununua mbolea, na alipelekwa hospitalini haraka mara baada ya hali yake kubadilika.

Mchungaji  Mwasomola aliongeza kuwa hawakutoa taarifa polisi kutokana na kuchanganyikiwa na tukio hilo, lakini Novemba 27 walipeleka taarifa katika Kituo cha Polisi Mlowo.

MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI