Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. George Simbachawene, amewasihi wananchi kudumisha amani na kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha usalama wa Taifa unaendelea kuimarika.
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo Novemba 25, 2025 katika ziara yake ya kutembelea baadhi ya vituo vya Jeshi la Polisi vilivyochomwa moto jijini Dar es Salaam, ikiwemo vya Ubungo, Temboni, Mbezi Juu na Salasala, kufuatia madhara yaliyotokana na vurugu za Oktoba 29, 2025.
Waziri amesisitiza kuwa uharibifu wa miundombinu ya vituo hivyo umekwamisha utendaji kazi wa baadhi ya vituo, jambo lililosababisha wananchi kushindwa kupata huduma za kawaida kupitia vituo hivyo.
Aidha, Mhe. Simbachawene amewaomba wananchi kuendeleza mshikamano na Polisi, akibainisha kuwa mshikamano huo ndio msingi wa kudumisha amani na usalama wa Taifa.
Ameongeza kuwa uharibifu wa mali za Serikali na wananchi si hasara kwa Taifa tu, bali pia ni upotezaji wa rasilimali muhimu zinazotumika kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha, Waziri amesisitiza kuwa Serikali imeanza hatua za haraka kuhakikisha miundombinu ya Jeshi la Polisi inarejeshwa kwa ufanisi, ili usalama wa wananchi udumishwe.
Vilevile, Mhe. Simbachawene amewaomba wananchi kudumisha mshikamano na Polisi na kushirikiana kwa karibu na Jeshi hilo ili kuhakikisha upendo, amani na utulivu wa jamii vinaimarishwa.









0 Comments