NA MATUKIO DAIMA MEDIA ,SINGIDA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba ameelekeza Jeshi la Polisi na Uhamiaji kuhakikisha wanamkamata na kuzuia hati ya kusafiria ya mkandarasi anayejenga mradi wa Kituo cha Ukaguzi cha Pamoja kilichopo Muhalala mkoani Singida.
Dk Mwigulu amesema kuwa mkandarasi huyo aliaminiwa na Serikali kwa kupewa ujenzi wa mradi huo wa kimkakati uliosimama kwa zaidi ya miaka nane tangu mwaka 2016. Mradi huo unaojengwa na kampuni ya Impresa di Costruzioni Ing. E. Mantovani S.p.A ulipaswa kukamilika mwaka 2018.
Ametoa agizo hilo leo Ijumaa tarehe 21 Novemba, 2025 wakati alipokagua mradi huo katika ziara yake ya kikazi mkoani Singida ambapo atakagua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.
Dk Mwigulu amesema kuwa jitihada zimefanyika za kuona mradi huo unaendelea lakini mkandarasi amekuwa akileta ugumu katika utekelezaji "Mkandarasi huyu alitangazwa amefilisika na hawezi kuendelea na mradi na alielekezwa ailipe fidia Tanzania kwasababu ameicheleweshea mradi"
"Naelekeza, Kamishna wa Uhamiaji kamata hati yake ya kusafiria, asitoke nje ya nchi mpaka jambo hili liishe, hii ni hujuma ya waziwazi, hii ni dharau ya waziwazi anaifanyia nchi yetu, Jeshi la Polisi mtafuteni mkandarasi huyu popote alipo, tumemuajiri, tunamlipa lakini anajiamulia Kama aendelee na kazi au asiendelee, huyu ni mhalifu akamatwe mpaka jambo hili liishe," amesisitiza Dk Mwigulu
Dk Mwigulu amesema kuwa makandarasi wa nje wanapaswa kufahamu kuwa wanapokuja kufanya kazi hapa nchini, watambue Tanzania imewaajiri na wasijione kama wao ni mabosi.






0 Comments