Na Samwel Mpogole-Mbeya.
Katika jitihada za kuboresha uzalishaji wa karoti na kuongeza ubora wa mazao yanayofika sokoni, Kampuni ya East West Seed imeendesha mafunzo maalumu kwa wakulima wa Mbeya kuhusu matumizi ya mbegu bora za karoti na mbinu za kisasa za uzalishaji.
Mafunzo hayo yalilenga kuwaandaa wakulima kuelekea msimu mpya wa kilimo, ambapo mahitaji ya karoti yenye ubora na zinazodumu muda mrefu sokoni yameendelea kuongezeka.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Kilimo wa East West Seed, Kelvin Ngonyani, alisema kampuni imebaini kuwa sehemu kubwa ya changamoto zinazowakabili wakulima wa karoti zinatokana na matumizi ya mbegu zisizo na ubora na kutofuata kanuni muhimu za uzalishaji.
“Tunataka kuona mkulima wa Mbeya anazalisha karoti zenye ubora unaokidhi soko la ushindani. Mbegu bora zina mchango mkubwa katika mavuno mengi, ukinzani wa magonjwa na muonekano mzuri wa karoti katika soko,” alisema Ngonyani.
Wakulima walifundishwa namna ya kupanda kwa spacing sahihi, utunzaji wa shamba, matumizi ya mbolea za kisasa, udhibiti wa visumbufu, pamoja na njia za kuvuna na kuhifadhi karoti bila kupoteza ubora.
Baadhi ya wakulima waliohudhuria mafunzo walisema elimu hiyo imewasaidia kuelewa tofauti kati ya mbegu za kawaida na mbegu za kisasa zinazotolewa na East West Seed, ambazo zinatajwa kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji.
Kwa upande mwingine, madalali wa mazao katika masoko ya Mbeya walisema karoti za ubora wa juu zimekuwa na soko kubwa, hasa zile zilizo sawa kwa umbo, zenye rangi nzuri na zisizoharibika haraka. Walisisitiza kuwa elimu kama hii inawawezesha wakulima kufikia viwango hivyo na kujiongezea kipato.
Mafunzo haya ni sehemu ya mkakati wa East West Seed kuhakikisha wakulima wanapata uelewa sahihi wa mbegu bora za karoti na jinsi zinavyoweza kubadilisha uzalishaji na maisha yao kiuchumi, huku wakihimizwa kutumia teknolojia za kisasa ili kwenda sambamba na mahitaji ya soko la leo.








0 Comments