Wananchi wa Mkoa wa Dar Es Salaam wanaoishi kwenye maeneo ambayo Usafiri wa mabasi yaendayo haraka maarufu kama Mwendokasi, yalitatizika na matukio ya Uvunjifu wa amani ya Oktoba 29, 2025, wameiomba serikali kurejesha huduma hiyo ya usafiri ili kuondokana na adha kubwa wanayoipitia.
Kwa nyakati tofauti leo Alhamisi Novemba 27, 2025 wananchi hao wameeleza adha kubwa wanayoipitia sasa ya kupanda magari zaidi ya mawili katika safari ambazo walikuwa wakitumia basi moja pekee la mwendokasi, huku pia gharama zake zikiwa kubwa na zikiongezeka zaidi kutokana na kuongezeka kwa mahitaji.
"Sasa hivi hakuna usafiri wa moja kwa moja, lazima uunganishe magari pamoja na bajaji na bahati mbaya bei imepandishwa, bado pia tunakaa muda mrefu kituoni." Amesema Khalid Mbwana, Mkazi wa Kimara.
Aidha wananchi hao pia wanaotumia barabara ya Morogoro, Kimara Mbezi, wameeleza namna ambavyo wanatumia muda mrefu barabarani kutokana na msongamano mkubwa wa magari kwenye barabara hizo, tofauti na mwendokasi ambapo kumekuwa na barabara zake yenyewe.
Ghasia na matukio ya Uvunjifu wa amani uliotokea siku ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 mbali ya kuharibu majengo na miundombinu ya watu binafsi, wahusika pia waliharibu mabasi na Vituo vya Mabasi ya mwendokasi, suala ambalo limesababisha serikali kusimamisha huduma hiyo ya usafiri ili kupisha tathmini na ukarabati.







0 Comments