Na Samwel Mpogole-Mbeya
Wajasiriamali wanaojishughulisha na mnyororo wa thamani wa zao la alizeti kutoka mikoa ya Mbeya na Songwe wamepata mafunzo maalum yanayolenga kuongeza uwezo wao katika biashara, masoko na udhibiti wa ubora.
Mafunzo hayo yameratibiwa na RIKOLTO kupitia mradi wa YEFFA kwa ushirikiano na TASUPA pamoja na FIT, yakikusanya wadau mbalimbali vijana wakiwemo wakulima, wakusanyaji, wasindikaji na wachakataji.
Mratibu wa Miradi kutoka Rikolto, Shukuru Tweve, alisema mafunzo hayo yameandaliwa ili kuwaendeleza wadau wa zao la alizeti hasa katika kuongeza ufanisi na ushindani wa bidhaa zao sokoni.
Aliongeza kuwa uelewa Kwa vijana kuhusu ubora ni nguzo muhimu katika kipindi ambacho sekta ya kilimo inaendelea kukua kwa kasi na mahitaji ya soko kubadilika.
Kwa upande wa TASUPA, Salma Mtoi ambaye ni Mtaalamu wa Chakula, alisisitiza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia wajasiriamali kuboresha ubora wa bidhaa zao tangu hatua ya uzalishaji shambani hadi zinapowafikia walaji.
Alisema kufuata kanuni bora za uzalishaji kunahakikisha bidhaa zinakuwa salama, zinakubalika na zinakidhi viwango vya udhibiti.
Akizungumzia kanuni hizo, Ladislaus Ikombe, Mkurugenzi wa Food Formation Tanzania ambaye ni mkufunzi katika mafunzo hayo, alitaja nguzo tano muhimu zinazopaswa kuzingatiwa ili kufanikisha uzalishaji wenye viwango bora. Nguzo hizo ni Watu, Bidhaa, Utaratibu, Eneo la Usindikaji, na Mchakato wa Uzalishaji.
Alifafanua kwamba uzingatiaji wa nguzo hizo husaidia kulinda usalama wa walaji na kuimarisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa.
Washiriki wa mafunzo wameeleza kuwa elimu waliyoipata imewapa uwezo mpya wa kuelewa masoko, kuboresha usalama wa chakula na kuongeza thamani ya zao la alizeti.
Wamesema mafunzo hayo yataongeza tija katika shughuli zao za kila siku na kuwapanua katika ushindani wa soko.
Mafunzo haya yanatarajiwa kuboresha mnyororo mzima wa thamani wa alizeti na kuchochea ukuaji wa uchumi wa vijana, kutoa ajira Kwa vijana ambao wapo katika mnyororo wa thamani wa alizeti kupitia mradi wa YEFFA wenye lengo la kufikia vijana takriban 100000









0 Comments