Header Ads Widget

UTAFITI WA MGODI MKUBWA WA DHAHABU WAANZA HANANG, WAZIRI MAVUNDE AONGOZA UKAGUZI

 


Na Matukio Daima Media


UUTAFITI wa kina wa madini ya dhahabu umeanza rasmi katika Kata ya Basotu wilayani Hanang mkoani Manyara, hatua inayotarajiwa kufungua njia ya kuanzishwa kwa mgodi mkubwa wa dhahabu katika eneo hilo. Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ametembelea eneo la mradi huo na kushuhudia utekelezaji wa utafiti unaofanywa kwa teknolojia ya ndege nyuki na kampuni ya SkyPM Solution.



Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyelitaja suala la utafiti wa madini kuwa kipaumbele cha Serikali kwa miaka 2025–2030, lengo likiwa kuongeza kiwango cha utafiti wa madini nchini kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kufikia angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.


 Akizungumza baada ya kukagua kazi hiyo, Waziri Mavunde amesema utafiti huo ni hatua muhimu katika kuchochea maendeleo ya wananchi wa Hanang na mkoa wa Manyara kwani matokeo yake yatafungua fursa za ajira, uwekezaji na miradi ya kijamii kupitia mapato ya leseni za uchimbaji.


Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mhe. Almish Hazal, amesema utafiti huo ni ishara ya matumaini mapya kwa wilaya yake na ameomba Wizara ya Madini kuendeleza juhudi hizo katika maeneo mengine yenye viashiria vya uwepo wa madini. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Cobra Resources Ltd, Bw. Amos Nzungu, ameipongeza Serikali kwa usimamizi wa karibu wa mradi huo na ameahidi kukabidhi matokeo ya utafiti pindi yatakapokamilika.

Akifafanua kuhusu teknolojia inayotumika, Meneja wa kampuni ya SkyPM Solution,  Paul Madata, amesema matumizi ya ndege nyuki yameongeza ufanisi wa utafiti kwa kuwa yana uwezo wa kuchunguza zaidi ya kilomita tatu chini ya ardhi kwa muda mfupi ikilinganishwa na mbinu za zamani.

Hata hivyo, Afisa Madini Mkazi wa Manyara, Mhandisi Godfrey Nyanda, amesema kuwa hadi robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26 mkoa huo umekusanya asilimia 35.21 ya lengo la makusanyo ya Shilingi Bilioni 2.2 na amesisitiza kuwa ofisi yake itaendelea kusimamia kikamilifu maelekezo ya Serikali ili sekta ya madini iendelee kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa mkoa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI