Header Ads Widget

WAZIRI NANAUKA ATAKA VIJANA WHUDUMIWE KWA KASI


Na Moses Ng’wat, Songwe.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amewataka watendaji wa serikali kuongeza kasi ya kuwahudumia vijana pindi wanapohitaji mikopo, ili waweze kukimbizana na fursa zinazojitokeza kwa wakati.


Akizungumza na wajasiriamali katika Soko Kuu la Mkwajuni wilayani Songwe, Novemba 26, 2025, Nanauka alisema kuchelewesha mikopo kwa miezi mingi kunawanyima vijana nafasi ya kunufaika na uwezeshaji wanaouhitaji kwa haraka.



Alisisitiza kuwa huduma zinazohusu vijana hazipaswi kuwa na urasimu bali wanapaswa kuhudumiwa kwa haraka bila vikwazo ili waweze kukimbizana na fursa zinazojitokeza kwa wakati.


Waziri huyo aliwataka watendaji kuwa wawazi kwa vijana, akisema ni vema kuwaambia mapema kama jambo haliwezekani badala ya kuwaacha wakisubiri huduma isiyopatikana ili vijana hao waweze kutafuta namna nyingine ya kupambania fursa zilizopo kwa wakati huo.


Aliongeza kwamba watendaji wanapaswa kuwafuata vijana walipo na kusikiliza changamoto zao, kwani sauti za wengi—ikiwamo ya kina Zakaria, mfanyabiashara mdogo sokoni hapo—hazifiki serikalini kutokana na urasimu.


Aidha, Nanauka aliwakemea watendaji wanaowambia vijana hawana vigezo bila kuwaelekeza namna ya kuvipata wanapoomba mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri, akisema serikali haitamvumilia yeyote atakayekwamisha jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwawezesha vijana.


Katika hatua nyingine, aliagiza halmashauri zote nchini kuwatambua vijana wanaojishughulisha na kazi mbalimbali katika maeneo yao, ili kuwasaidia kwa kuzingatia ujuzi na mahitaji yao, ikiwemo wale ambao hawakupata elimu ya darasani.


Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko hilo, Baraka Ndelwa, aliiomba serikali kuweka utaratibu rahisi utakaohakikisha mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa wakati.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Songwe, Cecilia Kavishe, alisema tayari halmashauri imetoa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 944 kwa vikundi 64 vyenye zaidi ya wanachama 300, na kwamba vikundi 22 vipo hatua za mwisho kupokea fedha wiki hii.


Waziri Nanauka amekamilisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Songwe ambapo amefanikiwa kukutana na kuzungumza na vijana wa makundi mbalimbali katika Halmashauri ya Mji Tunduma, Mbozi na Songwe, ambapo vijana bila kuwa na woga wamefunguka mambo mbalimbali ambayo yamekuwa kikwazo kwao kujinyanyua kiuchumi.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI