Header Ads Widget

TAASISI ZA KILIMO ZAASWA KUZALISHA KWA TIJA NA SIYO HASARA

 

Na Matukio Daima Media Dodoma

WAZIRI wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) amefanya kikao kazi na Bodi ya Kahawa Tanzania; Bodi ya Tumbaku Tanzania; Bodi ya Pamba Tanzania; na Bodi ya Sukari Tanzania na kuzitaka kuwa na mikakati endelevu ya kuzalisha mazao kwa tija, kutafuta masoko ya uhakika ili wakulima wanufaike kwa kuzalisha mazao kibiashara. 

Pia ameitaka Bodi ya Sukari kuwa na mfuko utakaojihusisha pia kugharamia shughuli za uendeshai wa Chuo cha Taifa cha Sukari (National Sugar Institute -NIS) ili kiweze kutengeneza mitaala inayoendana na ukuaji wa teknolojia ya sukari na viwanda.  Bodi ya Sukari nayo imeelekezwa kuja na mkakati wa kuongeza uzalishaji wa sukari katika kukidhi mahitaji nchini; huku pia kuanza kuzalisha ethanol kibiashara.



Waziri Chongolo ametoa maelekezo hayo tarehe 25 Novemba 2025 wakati wa Kikao Kazi chake na Wakurugenzi Wakuu wa Taasisi hizo, akiwemo Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Sukari (National Sugar Institute -NIS), jijini Dodoma.

Kuhusu Bodi ya Kahawa Tanzania, Waziri Chongolo ameitaka kutoa msukumo kwa AMCOS za zao la Kawaha ili ziwe na mashine za kutosha kukoboa Kahawa (primary processing) na kutenga bajeti ya kununua mashine hizo.  “Tukienda hivyo inakuwa mkulima anajitoa, na sisi Serikali tunajitoa ili kuhakikisha anapata tija kama mkulima wa Kahawa,” ameeleza Waziri Chongolo.


Kwa upande wa Bodi ya Pamba, Waziri Chongolo ameitaka ikae na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ili kuandaa na mikakati endelevu ya kuongeza uzalishaji wa mbegu zenye ubora; kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija katika zao hilo. 


“Tusizalishe hasara, bali tuzalishe tija na tuitafute kwa njia yoyote.  Hatuwezi kuendelea na mazingira yale yale.  Ni lazima kumlinda mkulima kwa kuonesha takwimu zenye tija,” amesema Waziri Chongolo. 

Aidha, Waziri Chongolo ameitaka Bodi ya Tumbaku Tanzania kupata teknolojia mbadala ya kukaushia Tumbaku kwa kutumia “solar” hususan kutoka katika nchi za China au Vietnam, huku akisisitiza wataalamu kutatua changamoto zozote kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji na masoko.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI