Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WAKUU wa shule za msingi kutoka mikoa 26 nchini wamekutana jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu wa Saba wa Chama cha Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania (TAPSHA), wakitoa maazimio na mapendekezo mazito kuhusu mustakabali wa elimu nchini.
Katika mkutano huo, viongozi hao wamesisitiza kuwa elimu ni huduma ya umma na siyo biashara, wakitaka uongozi wa elimu na Serikali kwa ujumla kuwekeza katika usimamizi, rasilimali watu na miundombinu ili kuongeza ubora wa elimu kwa watoto wa Kitanzania.
Mwenyekiti wa TAPSHA, Rehema Ramole, amesema viongozi wa shule wana wajibu wa kuhakikisha malengo ya Serikali katika sekta ya elimu yanatekelezwa ipasavyo, ikiwemo usimamizi wa mradi na utoaji wa huduma kwa wakati.
Amesema mkutano huo ni sehemu ya utaratibu wa kila mwaka wa viongozi wa ngazi ya taifa kukutana na kupitia changamoto na mafanikio ya sekta.
Akitoa maelekezo kwa washiriki wa mkutano, Profesa Shemdoe amewataka wakuu wa shule kusimamia kikamilifu uandikishaji wa wanafunzi ili kila mtoto mwenye umri wa kuanza shule apate nafasi.
Amesisitiza pia usimamizi wa miradi ya elimu na kuwataka viongozi wa shule kufuata miongozo yote ya Serikali.
Mkutano huo umeitaka TAMISEMI kuzingatia ajira kwa walimu waliokuwa wakijitolea, wakisema walimu hao wamechangia pakubwa katika kuboresha elimu katika maeneo yenye uhaba wa watumishi. Aidha, viongozi wa TAPSHA walitoa rai kwa wakurugenzi wa halmashauri kutenga bajeti ya upandishwaji wa madaraja, kusikiliza kero za watumishi na kuimarisha mawasiliano ya kiutendaji.
Katibu Mkuu wa TAPSHA, Odas Bambaza, amesema mkutano huo umeandaliwa kwa ajili ya kupokea maelekezo ya kitaifa na kuyageuza kuwa mpango-kazi unaotekelezeka.
Amesema chama hicho kimejipanga kuongeza tija na kuendelea kupeleka tabasamu kwa Watanzania kupitia utoaji wa elimu bora.
Mkutano huo pia umejadili hali ya shule binafsi, ambapo Serikali imeshauri wamiliki wa shule kupunguza ada ili kuongeza upatikanaji wa elimu kwa watoto kutoka familia zenye kipato cha chini.
Kwa mujibu wa viongozi wa TAPSHA, utoro mashuleni umepungua kwa kiwango kikubwa huku mazingira ya kujifunzia yakionekana kuboreka katika maeneo mengi nchini.
Maelekezo na mapendekezo yote yaliyotolewa katika mkutano huo yamekabidhiwa kwa katibu wa chama kwa ajili ya kuingizwa katika program ya utekelezaji ili kuhakikisha malengo ya kuboresha elimu nchini yanatimia.





0 Comments