Na Matukio Daima Media, Iringa
Diwani mteule wa Kata ya Lumuli, Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, Obedi Kisinini, ameonyesha mfano wa uongozi wenye kujali wananchi baada ya kununua gari la wagonjwa (ambulance) kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika kata hiyo.
Kisinini amesema kuwa kwa muda mrefu Kata ya Lumuli imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kukosa gari la wagonjwa kutokana na kutokidhi vigezo vinavyohitajika, hali iliyokuwa ikisababisha wagonjwa kusafirishwa kwa shida au kwa kutumia usafiri usio maalum.
Amesema hatua ya kulipatia kata yake ambulance hiyo imetekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, akisema ushirikiano huo umesaidia kufanikisha upatikanaji wa gari hilo la kisasa litakalotumika kwenye zahanati ya kata hiyo.
Aidha, diwani huyo ametoa wito kwa wadau wa afya kuendeleza ushirikiano wao katika kutoa elimu, ushauri na misaada mbalimbali ya kiafya, ili kuendelea kuokoa maisha ya wananchi, hususan wale wanaopoteza maisha kutokana na kukosa uelewa sahihi juu ya masuala ya afya.
Katika hatua nyingine, Kisinini amethibitisha kuwa tayari amechukua fomu ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa Vijijini na kwa sasa anasubiri vikao vya maamuzi ili kupitisha majina ya watakaogombea nafasi hiyo.
Kuwa gari hilo la wagonjwa linatarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma za dharura na kuboresha ustawi wa wananchi wa Kata ya Lumuli.







0 Comments