Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, ameiamuru Tume ya Madini kuchukua hatua za haraka kufuta leseni 73 za madini zinazomilikiwa na watu na kampuni zilizoshindwa kuziendeleza kwa mujibu wa sheria na masharti ya utoaji leseni hizo.
Akizungumza leo jijini Dodoma mbele ya waandishi wa habari, Mavunde amesema Serikali imechoshwa na tabia ya baadhi ya wawekezaji kuchukua leseni na kuzihodhi kwa miaka bila kuanza shughuli za uchimbaji, hali iliyosababisha maeneo makubwa kubaki bila maendeleo huku sekta ya madini ikihitaji uwekezaji wenye tija.
“Nimeielekeza Tume ya Madini kufuta mara moja leseni 73 ambazo hazina maendeleo yoyote sitavumilia watu au wawekezaji wanaochukua leseni na kuzifungia chumbani Leseni si pambo Ukichukua leseni lazima uende ukachimbe,” amesema Mavunde kwa msisitizo.
Amesema wamiliki wa leseni hizo wamekuwa wakikiuka masharti muhimu ya kisheria, ikiwemo kutowasilisha mipango ya maendeleo ya mradi, kushindwa kutekeleza masharti ya kifedha, kutoanzisha shughuli za utafiti au uchimbaji, na kuhodhi maeneo bila sababu za msingi.
“Huu ni uzembe na ni kikwazo katika kuongeza mapato ya Serikali, ajira kwa Watanzania na kuendeleza mnyororo wa thamani wa madini Tume ichukue hatua, sheria ichukue mkondo wake,” ameongeza.
Kwa mujibu wa Mavunde, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya madini pamoja na mifumo ya utoaji leseni, hatua iliyochangia ongezeko la idadi ya maombi mapya hata hivyo, alisisitiza kuwa uhitaji wa uwekezaji hauwezi kuwa sababu ya kuvumilia wamiliki wasiotekeleza wajibu wao.
Waziri huyo aliwataka wawekezaji wote wakubwa, wakati na wadogo kuhakikisha wanafuata masharti ya leseni zao, akisema kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua zaidi ikiwemo kufuta leseni nyingine zitakazobainika kukiuka sheria.
“Kila anayemiliki leseni katika nchi hii lazima afuate sheria tunataka sekta ya madini iwe na tija, iwe na matokeo, na iwe na mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa,” amesema.
Kufutwa kwa leseni hizo 73 kunatarajiwa kufungua njia kwa wawekezaji wengine wenye uwezo na nia ya kuendeleza maeneo ya madini yaliyokuwa yamekwama kwa muda mrefu.





0 Comments