Kongamano maalum la maendeleo ya mchezo wa kuogelea limefanyika hapo jana jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa michezo, makocha, wachezaji, wazazi, pamoja na wakurugenzi wa vituo vya mafunzo ya kuogelea. Tukio hilo limeibua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa mchezo huo nchini, hususan katika kipindi ambacho Tanzania imeonyesha nia ya dhati ya kuwekeza kwenye michezo kama nyenzo ya kuimarisha afya, ajira, na ustawi wa vijana.
Kongamano hilo, ambalo limeandaliwa na kampuni ya usimamizi wa michezo ijulikanayo kama Prime Sports Agency, lilijikita katika mada kuu tatu: ukuaji wa mchezo wa kuogelea nchini, changamoto zinazoukabili mchezo huo, na fursa zilizopo katika kuibua vipaji vipya kwa vijana wadogo. Washiriki walipata nafasi ya kuchangia mawazo kuhusu namna ya kuboresha miundombinu, uundaji wa programu maalum za kuibua vipaji, pamoja na kuongeza ushirikishwaji wa wazazi na shule katika kukuza mchezo huo kuanzia ngazi ya chini.
Akihutubia kama mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Ndg. Boniface Tamba, aliwapongeza waandaaji wa kongamano hilo na kusisitiza umuhimu wa kuwepo kwa majadiliano ya mara kwa mara kati ya wadau ili kuleta mabadiliko chanya yenye tija kwa taifa.
“Kongamano kama hili liwe sehemu ya utaratibu endelevu, siyo tukio la mara moja. Lazima tuwe na mwendelezo wa kuzungumza, kupanga na kutekeleza. Maendeleo ya michezo nchini, ikiwemo kuogelea, hayawezi kutokea kwa bahati nasibu bali kwa mikakati thabiti,” alisema Ndg. Tamba.
Mkurugenzi huyo alisisitiza pia kuwa mipango itakayowekwa na wadau hao ni lazima iendane na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akihimiza usimamizi imara, utafutaji wa rasilimali, na matumizi ya takwimu katika kupanga maendeleo ya michezo.
“Wasimamizi wa mchezo huu wanapaswa kuja na mpango mkakati utakaowezesha kuogelea kuwa miongoni mwa michezo inayotoa ajira, medali, na fursa kwa vijana wetu. Lazima tuweke malengo makubwa kama taifa,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Prime Sports Agency ambayoinahusika na mambo ya usimamizi wa michezo, Bwana Lameck Borega, ambaye taasisi yake ndiyo mwandaaji mkuu wa kongamano hilo, aliwataka washiriki kuzingatia yale yote yalijadiliwa badala ya kuishia kuyasikia tu. Alisema kuwa mijadala iliyofanyika inapaswa kuwa dira ya mabadiliko kwa wadau wote wa mchezo huo.
“Tumeyajadili mengi hapa leo. Sasa ni jukumu letu kuyageuza kuwa mwongozo wa vitendo. Wadau wa kuogelea wanapaswa kuwa mfano wa nidhamu, umoja na ubunifu. Tukifanya hivyo, tutafika mbali,” alisema Borega.
Aidha washiriki mbalimbali walieleza changamoto zinazolikabili eneo hilo la michezo, ikiwemo upungufu wa mabwawa ya viwango, ukosefu wa vifaa vya kisasa vya mafunzo, gharama kubwa za uendeshaji wa klabu za kuogelea, pamoja na uhitaji wa kozi za mara kwa mara kwa makocha na waamuzi. Wengine walipendekeza kuanzishwa kwa mashindano ya mara kwa mara katika mikoa mbalimbali ili kutambua na kukuza vipaji nchini.
Kongamano hilo limehitimishwa kwa kutoa mwito kwa serikali, sekta binafsi, na wadau wa elimu kushirikiana kwa karibu ili kuwezesha vijana kushiriki katika mchezo wa kuogelea tangu wakiwa shule za msingi. Washiriki walisisitiza kuwa upo uwezekano mkubwa wa Tanzania kuzalisha mabingwa wa kimataifa iwapo kutakuwa na uwekezaji wa kimkakati.
Tukio la jana limeelezwa kuwa mwanzo mpya katika safari ya kuufanya mchezo wa kuogelea kuwa sekta yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya michezo nchini. Prime Sports Agency imethibitisha kuwa mafanikio ya kongamano hilo yamefungua milango ya kuandaa makongamano mengine makubwa zaidi siku zijazo ili kuendelea kujenga msingi imara wa mchezo huo.









0 Comments