Header Ads Widget

MIKOKO YAPEWA KIPAUMBELE KITAIFA



_Waziri: Hekta 158,000 za hifadhi zilindwe, ziwe ngao ya mabadiliko ya tabianchi_


Na Mwandishi Wetu, Lindi

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe Dkt. Ashatu Kijaji, amezindua kwa vitendo kampeni ya kitaifa ya upandaji miti kwa kupanda mikoko 1,020 katika fukwe za Machole, mkoani Lindi, akisisitiza umuhimu wa kulinda zaidi ya hekta 158,000 za misitu ya mikoko nchini kama nguzo ya uchumi na kinga dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.


Akizungumza leo Machi 18, 2026 katika tukio la Siku ya Mikoko, moja ya matukio ya awali kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani yatakayofanyika Machi 21, Waziri Kijaji alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na mikoko kuanzia Tanga hadi Mtwara, lakini uhifadhi wake unahitaji ushirikiano wa wadau wote.


“Mikoko ni muhimu kwa uchumi na uhai wa dunia. Ina uwezo mkubwa wa kufyonza hewa ukaa kuliko aina nyingine nyingi za misitu, hivyo ni silaha muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema.


Aliongeza kuwa mbali na kuchangia kupunguza athari za tabianchi, mikoko ni mazalia ya samaki na viumbe wengine wa baharini, hivyo uharibifu wake ni tishio kwa usalama wa chakula na uchumi wa jamii za pwani.


“Mikoko inalinda fukwe dhidi ya mmomonyoko kwa kupunguza nguvu ya mawimbi. Maeneo yenye mikoko imara hayakabiliwi na mmomonyoko mkubwa,” alisisitiza.


Katika tukio hilo lililoshirikisha viongozi wa serikali, wadau wa mazingira na wananchi, Waziri huyo aliupongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kazi ya kusimamia na kulinda rasilimali hiyo, akitoa wito wa kuendeleza juhudi hizo sambamba na kampeni ya kitaifa ya upandaji miti iliyoanzishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan chini ya ajenda ya “Tanzania ya Kijani.”


Aidha, aliwataka wananchi wa Lindi na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi katika ufunguzi wa maadhimisho hayo utakaofanyika kesho Machi 19, 2026 katika Uwanja wa Ilulu, yakitarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe Dk Emmanuel Nchimbi.


Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali TFS, Dkt. Zainabu Shaban Bungwa, alisema mikoko ina spishi tisa zinazotambulika kitaalamu nchini, huku akibainisha kuwa mti uliopandwa na Waziri ni Rhizophora mucronata, maarufu kama mkoko.


Alieleza kuwa mikoko ina uwezo mkubwa wa kufyonza hewa ukaa ambapo hekta moja inaweza kunyonya kati ya tani 800 hadi 1,200 za hewa ukaa, kiwango kinachozidi mara kadhaa miti ya kawaida inayonyonya kati ya tani 160 hadi 300.


Akitoa maelezo ya kitaalamu, Mhifadhi Mkuu mstaafu wa TFS ambaye kwa sasa ni Meneja wa Mradi wa BENGO, Frank Sima, aliyewasilisha kwa niaba ya Katibu wa Sekretarieti ya Mtandao wa Mikoko wa Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi (WIOMN), alisema katika tukio hilo zilipandwa spishi nne za mikoko ambazo ni Rhizophora mucronata, Avicennia marina (mchu), Bruguiera gymnorhiza (msinzi) na Ceriops tagal (mkandaa).


Alibainisha kuwa upandaji huo umefanyika kwa kufuata viwango vya kitaalamu kwa kutumia nafasi ya mita mbili kwa mbili katika mfumo wa zigzag ili kuongeza ufanisi wa ukuaji, ukihusisha eneo la takriban hekta 0.5.


Tukio hilo pia lilihudhuriwa na viongozi wa Mkoa na Wilaya ya Lindi wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe Victoria Mwanziva, Mbunge wa Mchinga, Mhe Salma Kikwete pamoja na wadau wa kimataifa wa uhifadhi wakiwemo IUCN, taasisi ya Mwambao Coastal Community Network, EarthLung na wadau wa maendeleo ya Bahari ya Hindi.


Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika wakati Tanzania ikiendeleza mikakati ya kimataifa ya uhifadhi na urejeshaji wa misitu, ikilenga kuongeza uoto wa asili, kulinda bioanuai na kuchochea uchumi wa kijani kupitia utalii wa mazingira na rasilimali misitu.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI