Na. Calvin Katera - Same.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii Timotheo Mnzava amesema yeye pamoja na Kamati anayoiongoza wameridhishwa na utekelezaji wa miradi miwili ya uzalishaji wa faru weusi pamoja na mbwamwitu, wanyama waliokuwa hatarini kutoweka katika uso wa dunia kutokana na ujangili uliokithiri miaka ya 1980 hadi 1990.
Mradi wa faru weusi ulioanzishwa mwaka 2018 na kukamilika mwaka 2021 ndani ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi umeendelea kuwa kichocheo cha kuongezeka kwa wanyama hao adimu wanaowindwa kwa sababu ya pembe zao.
Aliyasema hayo leo machi 15, 2026 walipotembelea miradi hiyo na kujionea ongezeko la idadi ya wanyama hao pamoja na kazi za ulinzi wao unatekelezwa kwa njia ya TEHAMA na njia za kawaida ili kuendelea kuwa na idadi kubwa kwa mustakabali wa uchumi wa Taifa la Tanzania.
Akizungumza katika ziara hiyo Mnzava alisema " Mradi huu unatoa matumaini ya uhifadhi na utalii na unaridhisha kwakuwa unaongeza mazao ya utalii na pato kwa Taifa kupitia shughuli za utalii. Mradi huu tuliotembelea leo umeonyesha ni kwa namna gani shughuli za uhifadhi na utalii hufanyika kwa uzalendo mkubwa na ujasiri, kwa kujituma kuwalinda wanyamapori na vivutio vingine visiharibiwe ndani ya maeneo yote ya hifadhi".
Kwa upande wake Waziri Wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alisema kuwa Wizara itaendelea kuboresha miundombinu, vitendea kazi na mifumo ya usalama hifadhini ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kupitia mifumo mipya ya tehama na teknolojia katika kukabiliana na vitendo vya ujangili na uharibifu wa rasilimali zinazochangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya sekta ya utalii nchini.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas alisisitiza kuwa uwepo wa mradi huu kumefungua fursa zaidi za uwepo wa miradi mingine na mazao mapya ya utalii hususani mbwamwitu. Pia aliongeza kuwa Wizara itaendelea kuwatambua wale wote wanaofanya uhifadhi kwa kiwango cha juu kwa kuwapa wanyama majina yao ili kutunza kumbukumbu ya mchango wao katika sekta hii kama vile faru Fausta, faru Waitara na Faru Azam.
Aidha, Katibu Tawala Wilaya ya Same Mamdolwa Gembe alieleza kuwa wilaya inajivunia kuwa na Hifadhi kwani imekuwa chachu ya fursa za kiuchumi na imefungua milango ya shughuli za kiutalii kwa wageni na wazawa. Aliongeza kuwa uwepo wa Hifadhi hii kumepelekea kuanzishwa kwa Same Utalii Festival inayofanyika kila mwaka, tukio ambalo linawapa fursa watanzania wote kutembelea vivutio vilivyomo wilayani hapo.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Eva Mallya alieleza kuwa mradi huo unatakribani faru hamsini (50) na mbwamwitu kumi na mbili, baada ya wale wa awili kuwatawanya katika hifadhi nyingine nchini, na sasa wanyama hao wamekuwa ni kivutio kikubwa kwa watalii wa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.


















0 Comments