Header Ads Widget

WATANZANIA UGHAIBUNI WATAKIWA KUTOZUIA USHIRIKI WA WENGINE KATIKA UCHAGUZI

Na Shemsa Mussa -Matukio Daima Media 

 Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Watanzania Waishio China (DITAG), Ndg. Allawi Abdallah, ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuacha mara moja tabia ya kuwashawishi ndugu zao waliopo Tanzania kutojitokeza kupiga kura wakati wa uchaguzi. Amesema kupiga kura ni haki ya msingi na wajibu wa kila Mtanzania katika kujenga taifa la kidemokrasia.



Akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Kagera Ndg. Allawi amesema kuwa kuna baadhi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi ambao wamekuwa wakieneza propaganda za kuwakatisha tamaa Watanzania waliopo nyumbani kushiriki katika uchaguzi,huku akisema  kuwa tabia hiyo ni hatari kwa maendeleo ya taifa na inalenga kudhoofisha misingi ya demokrasia.


“Watanzania walioko nje ya nchi wanapaswa kuwa mabalozi wa maendeleo na siyo chanzo cha kuvuruga ustawi wa kisiasa wa nchi. Kupiga kura ni jukumu la kila raia na hakuna sababu ya kuwakatisha tamaa watu wetu,” amesema Ndg. Allawi.






Aliongeza kuwa nchi haiwezi kusonga mbele bila ya ushiriki wa wananchi katika maamuzi ya kisiasa kupitia sanduku la kura,amesema nchi nyingine duniani raia wake huona fahari kushiriki uchaguzi, na kuwahimiza Watanzania kuwa na moyo huo huo wa kizalendo.


Amewataka Watanzania kutumia fursa ya uchaguzi kufanya maamuzi yenye tija kwa taifa kwa kuchagua viongozi wanaowajali na wenye dira ya kweli ya maendeleo. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwaelimisha vijana kuhusu haki yao ya kupiga kura na kuwahimiza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.


Ndg.Allawi amewataka jamii nzima na mashirika ya kiraia kushirikiana katika kuwahamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi, huku akiahidi kuwa jumuiya ya Watanzania waishio China itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za kukuza demokrasia nchini Tanzania.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI