Na Shemsa Mussa -Matukio Daima Media.
Kagera.
Vijana nchini wametakiwa kutumia nafasi yao kama nguzo kuu ya taifa katika kulinda amani na kuhamasisha ushiriki wa wananchi kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kampeni ya (MAMA ASEMEWE) ambaye pia ni Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Geofrey Kiliba, wakati wa mkutano wa hamasa kwa vijana uliofanyika Katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
Kiliba amesema ni wajibu wa vijana kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani, haki na umoja, akisisitiza kuwa kundi hilo lina mchango mkubwa katika kulinda misingi ya demokrasia na maendeleo ya nchi.
“Amani ya taifa letu inaanzia kwa vijana. Tukisimama pamoja, tukahamasishana na kushiriki kwa utulivu, tutaandika historia ya uchaguzi wa mfano ” amesema Kiliba.
Kwa upande wao, baadhi ya vijana waliokuwepo katika mkutano huo wameahidi kuwa mabalozi wa amani kwenye jamii zao, wakiahidi kutumia ubunifu na mitandao ya kijamii kueneza ujumbe wa upendo na mshikamano kuelekea uchaguzi Mkuu.
Aidha, vijana hao wameishukuru serikali na vyombo vya ulinzi kwa kuendelea kudumisha utulivu wa nchi, huku wakiwataka Watanzania wote kujitokeza kwa wingi kupiga kura, wakisisitiza kuwa uchaguzi wa amani ni msingi wa maendeleo endelevu.
0 Comments