Na Moses Ng’wat, Songwe.
WATU wasiojulikana wamechoma moto nyumba ya Polisi Kata wa Kata ya Chitete, iliyopo Kijiji cha Ikumbilo, Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea usiku wa Oktoba 22, 2025, wakati askari huyo akiwa kwenye majukumu maalum.
Kamanda Senga alisema nyumba hiyo inamilikiwa na Mkaguzi wa Polisi, Nsajigwa Mwajeka, ambaye ni Polisi Kata wa eneo hilo, na kwamba moto huo uliteketeza vitu kadhaa kwenye vyumba viwili na uligunduliwa na Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Darkson Kamendu.
Amesema vitu vilivyoteketea katika nyumba hiyo ni pamoja na nguo za kiraia, sare za polisi, vyombo kadhaa, mahindi, kitanda, godoro, pamoja na vitu vingine vidogo, vyote vikiwa na thamani ya takribani shilingi milioni mbili.
“Chanzo cha tukio bado kinachunguzwa, lakini inaonyesha wahalifu walikusanya vitu na kuviweka kitandani kisha kuchoma moto kwa kutumia njiti za kiberiti zilizokutwa eneo la tukio,” alisema Kamanda Senga.
Hata hivyo, Kamanda Senga alisema kuwa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa, japo kuna watu wanaendelea kufuatiliwa na pindi watakapokamatwa jeshi hilo litatoa taarifa kamili.





0 Comments